Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limethibitisha kutokea kwa ajali mbili za Ndege ( muda tofauti) leo katika uwanja wa Ndege wa Kikoboga uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambapo zaidi ya Watu 60 kwenye Ndege zote mbili wamenusurika.
TANAPA imesema Ndege ya kwanza ya Unity Air 5H-MJH aina ya Embraer 120 majira ya saa 3:40 asubuhi ikiwa na Abiria 30, Marubani wawili na Mhudumu mmoja ikitokea Zanzibar ilipata tatizo la kiufundi wakati wa kutua kiwanjani hapo lakini kwa juhudi kubwa za Marubani na Maafisa wa kiwanja hicho hakuna madhara yaliyojitokeza ambapo Abira wote, Marubani na Muhudumu mmoja wako salama na wanaendelea na ratiba yao ya Utalii hifadhini.
Katika taarifa ya pili, TANAPA imethibitisha kutokea kwa ajali ya pili leoleo saa 9:30 alasiri ikihusisha Ndege ya Kampuni ya Unity Air 5H-FLM aina ya E120 ikiwa na Abiria 30, Marubani wawili na Wahudumu wawili iliyopata ajali wakati wa kuruka katika kiwanja hicho ikielekea Zanzibar ambapo hata hivyo hakuna aliyejeruhiwa katika ajali hiyo ambayo chanzo chake bado hakijafahamika.
“TANAPA ikishirikiana na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro na Wadau wa Utalii na usafiri wa anga wanaendelea kushughulikia mabadiliko ya mipango ya safari za Watali husika ili kupunguza adha iliyojitokeza, maeneo ya ndege kuruka na kutua katika kiwanja hicho hayajaathirika hivyo kiwanja kinaendelea kuwa wazi kwa safari za ndege na shughuli za utalii”
“TANAPA imefanya taratibu zote za mawasiliano na idara ya uchunguzi wa ajali za ndege iliyopo Wizara ya Uchukuzi -(AAIB) kwa ajili ya uchunguzi wa matukio tukio hili, Shirika linapenda kutoa shukrani kwa kikosi cha zimamoto na uokoaji Mikumi kwa ufanisi mkubwa katika changamoto hii” ——— imeeleza taarifa ya TANAPA.