NJOMBE,Takribani watu 185 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho katika hospitali ya wilaya ya Wangingombe mkoani Njombe bila kuchangia gharama yoyote baada ya shirika lisilo la kiserikali la Hellen Keller International kufadhili matibabu hayo.
Wakazi hao akiwemo Yusta Ndetewale,Luth Matandala na John Pondamali wamekiri kuanza kuona tena baada ya kutoona kwa miaka mingi huku wakitumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya Tanzania.
“Nimepata watoto nikiwa na ulemavu lakini wakati nasikia ujio wa matibabu haya ukanifanya nije ,madaktari wametibu sasa naona ,nawaona wote nyie ,alisema Luth Mtandala “
Dokta Frank Chiduo ni Mganga mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe ambaye anasema mpango huo umesaidia watu wengi kupatiwa huduma ya upasuaji wa macho hususani wazee ambao hupata changamoto ya macho kutokana na umri wao.
Naye Dokta Saada Ludovick Daktari bingwa wa macho toka Wizara ya Afya amesema kuna takribani watu milioni 3 wenye tatizo la macho nchini kote na ndio maana wamelazimika kuanza kutoa huduma hiyo kwenye kila Hospitali za rufaa za mikoa
Meneja mradi wa Shirika la Hellen Keller International Athuman Tawakali amesema mradi huo ni wa mwaka mmoja unaotarajiwa kuwafikia takribani watu 900 huku katika awamu ya kwanza wakitarajia kuwahudumia watu 300 wenye tatizo hilo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe Claudia Kitta ametembelea kambi hiyo katika hospitali ya wilaya hiyo iliyopo katika kijiji cha Ihanja ambapo amekiri kufanyika kwa kazi kubwa ya kuwatibu wananchi wake na kulazimika kutuma salamu kwa Rais wa Tanzania pamoja na Shirika hilo.