Na Sophia Kingimali
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amekitaka kituo cha huduma kwa mteja(Call Center)TANESCO kuandaa mikakati itakayosaidia kufanya wateja wote wanaopiga simu waweze kuhudumiwa.
Hayo ameyasema leo Novemba 27, 2023 jijini Dar es salaam alipotembelea kituo hicho cha huduma kwa mteja ili kujionea utendaji kazi wa kituo.
Amesema kumekuwa na mapungufu mengi katika shirika hilo huku moja wapo likiwa ni huduma kwa mteja kwani kwa siku zinapigwa simu 40,000 na zinazopokelewa ni simu 12,000 tu jambo ambalo linafikirisha na kupelekea kuangalia namna bora ya kuboresha huduma ili kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma hiyo.
“Niwaelekeze kitengo cha huduma kwa mteja TANESCO wahakikishe ndani ya muda mfupi waje na mikakati amabayo itawafanya wateja wote waweze kusikilizwa na changamoto zao kutatuliwa kwa wakati”amesema Kapinga.
Aidha ameongeza kuwa changamoto ambazo ni sugu kwenye shirikika hilo zinapaswa kutatuliwa kwa haraka ili kuendana na kasi ya teknolojia iliyopo.
Amesema changamoto zinaposhindwa kupatiwa suluhu kuna mambo mawili aidha shirika limeshindwa au waliopewa jukumu hilo wameshindwa hivyo itailazimu serikali kutafuta wengine kwani kwa karne hii swala la huduma kwa mteja halipaswi kuwa kikwazo.
Amesema pamoja na kuwa na changamoto ya umeme lakini mteja hapaswi kuwa na mawazo kwa ajili ya kushindwa kusikilizwa changamoto yake kwani mtu anapopata changamoto anapaswa kutatulia kwa muda wa saa tatu mpaka nne.
“Kwa takwimu za sasa hivi asilimia 32 wanahudumiwa kati ya saa tatu mpaka nne lakini asilimia 52 wanahudumiwa ndani ya saa nane niwaambie tu tulipofikia sasa umeme sio anasa umeme ni swala la msingi kwa kila mtanzania huwezi kumuacha mteja saa 12 hana umeme kwa sababu umeshindwa kwenda kumtatulia changamoto yake mgao ni kitu kingine na kumtatulia mteja changamoto yake ni jambo lingine”amesisitiza Kapinga.
Pia amewataka kuhakikisha wanawalipa stahiki zao wafanyakazi wote wa kituo hiko ili waendelee kuto huduma bora na stahiki kwa mteja na amewataka watoa huduma kutambua kuwa mteja ni mfalme hivyo wanapaswa kumuhudumia kwa nidhamu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa mteja Martine Mwambene amesema wamepokea maelekezo yote na watayafanyia kazi kwa wakati.
“Tumepokea maelekezo na tutayafanyia kazi kwani tayari tumeshaanza kuandaa mitandao mbalimbali ambayo tunaweza kuwasiliana na mteja ikiwemo mitandao ya kijamii lakini pia kwa kutumia SSD CORD”amesema Mwambene