Na. Anangisye Mwateba-Moshi Kilimanjaro
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amewaasa wahitimu wa chuo cha usimamizi wa wanyapori kuchukia rushwa, kutojitajirisha na hali ngumu za wananchi na walinde maliasili za nchi kwa wivu mkubwa na kuwa Walinzi wa wenzao.
Mhe. Biteko Amesema hayo wakati wa kutunuku vyeti vya ngazi mbalimbali kwa wahitimu 439 wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mweka akiwa amemuwakilishaRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 na Mahafali ya 59 ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, mkoani Kilimanjaro.
“Chuo hiki ni kiungo muhimu katika Sekta ya Maliasili na Utalii, kuanzishwa kwake kulitokana na tamko la Baba wa Taifa, Hayati, Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Kongamano la Uhifadhi wa Wanyama Pori mwaka 1961, na kupitia tamko hilo alionesha dhamira na utayari wake wa kuifanya Afrika kuwalinda wanyama na mazingira yao kwa kizazi kilichopo na vizazi vijavyo, hivyo nyinyi ndio mnaoendeleza kazi lengo hilo la Baba wa Taifa.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, Chuo hicho pia ni kielelezo cha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani kwani Chuo hicho kinapata wanafunzi kutoka nchini mbalimbali duniani.
Amesema kuwa, Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua mchango wa Chuo hicho katika ukuaji wa Sekta ya Maliasili na Utalii nchini na hivyo ameahidi kuwa kama kuna changamoto zozote Serikali itazichukua na kuzifanyia kazi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kusimamia vyema sekta ya Maliasili na Utalii ambayo amesema kuwa ni kiungo kikubwa kwenye uchumi wa nchi kwani bila Sekta hiyo mapato na fedha zinazohitajika kuendeleza miradi mbalimbali zinaweza kuwa na changamoto ya upatikanaji.
Amesema kuwa, Utalii unachangia takriban asilimia 21 ya Pato la Taifa, na asilimia 25 ya fedha za kigeni, pia ni chanzo kikubwa cha ajira nchini kwani unachangia ajira milioni 1.5 na zaidi ya asilimia 11 ya ajira zote hapa nchini.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa, asilimia 80 ya Utalii nchini unatokana na Wanyama pori, ambao wametokana na mazingira yetu tuliyoyoyahifadhi, mapori ya akiba, mapori tengefu, misitu pamoja na hifadhi za wanyama.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassani kwa msaada mkubwa anaoutoa katika Chuo cha Mweka kwa kukarabati, kununua vitendea kazi ambapo kwa sasa kuna ujenzi wa jengo kubwa la mafunzo ambalo gharama yake kiasi cha shilingi blioni 3.8.
Mhe. Kitandula alimalizia kwa kusema kuwa uongozi wa wizara utafanya kila linalowezekana kuendelea kuimarisha vyuo vilivyo chini ya wizara ya Maliasili na utalii vinakuwa bora na kutoa wahitimu wenye weledi wa hali ya juu.