Na Eleuteri Mangi, WUSM
Tanzania imeendelea kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuandaa mashindano ya tamasha la watu wenye usikivu hafifu (viziwi) la 2024 ambalo linatarajiwa kufanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni hifadhi Bora Zaidi Barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro usiku wa kuamkia Novemba 26, 2023 jijini Dar es salaam wakati akihitimisha tamasha hilo ambalo limefanyika kwa mara ya pili nchini Tanzania.
“Serikali ya Tanzania inawakaribisha kwa mara nyingine tena, Tanzania ni nchi ya amani na yenye vivutio vingi vya utalii, tamasha lijalo litafanyika katika hifadhi yetu ya Taifa ya Serengeti ambayo imeshinda kuwa hifadhi Bora zaidi Barani Afrika kwa mara ya Tano mfululizo. Nchi yetu inathamini haki za watu wote na makundi yote, ulemavu sio mwisho wa maisha, tutaendelea kushirikiana nanyi wakati wote” amesema Dkt. Ndumbaro.
Katika mashindano hayo, Nashua Patience kutoka Uganda ameibuka mshindi wa kwanza na kutwaa taji la mrembo kwa mwaka 2023 huku nafasi ya mtanashati katika mashindano hayo ikinyakuliwa na Ariko David kutoka Uganda wakati Mtanzania Caroline Mwakasaka akiibuka mshindi wa nafasi ya pili kwa upande wa shindano la Mwanamitindo Bora “modal”.
Kufanyika kwa mashindano hayo kwa mara ya pili mfululizo nchini Tanzania ni fursa kwa jamii hiyo kujitangaza kwa watu wote duniani bila kujali changamoto walizonazo pamoja na kutangaza vivutio vya Tanzania kupitia jamii ya viziwi kote duniani.
Akimkaribisha Waziri Dkt. Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Gerson Msigwa amesema Tanzania ipo tayari kuendelea kupokea mashindano hayo mwaka 2024 akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya upendo, utulivu na amani huku akibainisha kuwa kupitia Tamasha hilo Watanzania wamenufaika na kujifunza mambo mengi yaliyooneshwa na jamii hiyo kupitia ubunifu, vipaji, umoja na Mawasiliano kupitia lugha ya alama.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi. amesema Serikali imeunda wizara mahususi ili kusimamia watu wenye ulemavu na kujenga vyuo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu ili kuwapa ujuzi utakaowasaidia katika maisha yao.
Amesema Serikali inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan imefufua vyuo vya watu wenye ulemavu kwa gharama ya shilingi billion 3.4, imetoa fedha kiasi cha Sh. Bilioni 3 ili kujenga vyuo vipya vya ufundi vya watu wenye ulemavu kwa lengo la kupata elimu, ujuzi na mafunzo stadi.
Aidha, amesema kila mwaka Serikali inatenga kiasi cha zaidi ya milioni 60 kwa ajili mafuta kwa watu wenye changamoto ya ngozi pamoja na kututoa fedha za kukarabati mabweni katika halmashauri 50 nchini kwa gharama ya Sh. Bilioni 4 ili watu wenye ulemavu wapate haki na stahiki zao,
Naye rais wa Chama cha Viziwi Afrika na Tanzania Habibu Mrope pamoja na Bi. Bonita Ann Leek Mkurugenzi wa Miss na Mr Deaf International (MMDI) wameishukuru Tanzania ambayo inaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwa wenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya pili hatua inayowatia nguvu na hamasa watu wenye usikivu hafifu.
Tamasha hilo limehusisha washiri zaidi ya 200 kutoka mataifa ya Afrika Kusini, Australia, Belarus, Brazil, Ethiopia, Falme za Kiarabu, Guyana, Haiti, Hispania, India, Iran, Italia, Kenya, Kongo DRC, Malasia, Macedonia, Marekani, Mexico, Misri, Morocco, Msumbiji, Nigeria, Pakistan, Poland, Romania, Rwanda, Senegal, Siera Leone, Sudan Kusini, Thailand, Tunisia, Jamhuri ya Czechoslovakia, Ufaransa, Uganda, Ujerumani, Ukraine, Urusi, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.