Timu ya AICC iliyoshiriki kwenye mashindano ya Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni binafsi (SHIMMUTA) imeendeleza ubabe kwenye mchezo wa vishale (darts) kwa kuchukua ushindi kwa wanawake kupitia kwa mchezaji wake Eliasenya Nnko.
Michezo hiyo iliyohitimishwa leo kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma kwa mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Sitaki Senyamule ambaye alimuwakilisha Dkt. Damas Ndumbaro alitoa zawadi kwa Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni binafsi yaliyoshinda kwenye Michezo mbalimbali.
Mbali na kushiriki mchezo wa vishale, timu ya AICC ilishiriki michezo ya pooltable, riadha, bao, karata, darts na mbio za magunia na kufikia hatua mbalimbali ikiwemo hatua za nusu fainali.
Mashindano hayo ya SHIMMUTA yenye kauli mbiu “Michezo ni Afya na Uchumi: tuwekeze kwenye Miundombinu ya Michezo kwa Afya Bora na Uchumi Himilivu! Kazi Iendelee” yalianza tarehe 12 Novemba 2023 na kufunguliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko tarehe 17 Novemba 2023 kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.