Kutokana na mafanikio ya misako na doria zilizofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha kuanzia Novemba 13 hadi 23, 2023 na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 25 kwa tuhuma za makosa mbalimbali, wananchi wa mkoa huo wamelipongeza Jeshi hilo kwa utendaji wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Novemba 24, 2023 katika kituo kikuu cha Polisi Mbeya mara baada ya kutambua mali zao zilizoibwa na watuhumiwa wa matukio ya uvunjaji nyumba, makanisa na maduka, wananchi hao wamelipongeza Jeshi la Polisi.
Rose Eliud ni mkazi wa Jijini Mbeya ameeleza kuwa, Novemba 18, 2023 majira ya usiku wahalifu walivunja nyumbani kwao na kuiba televisheni, king’amuzi na”heater” ya kuchemshia maji lakini baada ya kutoa taarifa Jeshi la Polisi lilifanya ufuatilia na kukamata watuhumiwa na mali hizo.
Naye, Evance Rwemamu mkazi wa Jijini Mbeya amelipongeza Jeshi la Polisi kutokana na kufanikisha kupata mali zake zilizoibwa ambazo ni televisheni aina ya Hisense yenye ukubwa wa inchi 75 pamoja na vifaa vingine.