WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapongeza wataalamu kutoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kuokoa sh. bilioni 2.3 zilizokuwa zimepangwa kutumika kwenye mradi wa maji Itumba – Isongole wilayani Ileje, Mkoani Songwe.
“Ninawapongeza wataalamu wa RUWASA kwa usimamizi mzuri wa fedha za mradi wa maji wa Itumba – Isongole na kuweza kutekeleza mradi huo kwa gharama ya sh. bilioni 2.6 kati ya sh. bilioni 4.9 zilizokuwa zimetengwa. Mmebakiza fedha ya Serikali ambayo itatekeleza miradi mingine ya maji,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa pongezi hizo jana (Alhamisi, Novemba 23, 2023) mara baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la mradi huo ambao una lengo la kufanya maboresho ya miundombinu ya maji ili kuongeza kiwango cha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa mji wa Itumba na Isongole.
“Ninawapongeza Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso na Naibu wake, Mhandisi Mary-Prisca Mahundi kwa usimamizi mzuri. Nataka kusisitiza kuwa ni vema watekelezaji wa miradi ya Serikali wakajenga utamaduni wa uzalendo na uadilifu katika matumizi ya fedha za umma kama walivyofanya wenzetu wa RUWASA.”
Amewataka watumishi wa taasisi na mashirika ya umma yanayotekeleza miradi mbalimbali kote nchini wawe na uzalendo na waweke mbele maslahi ya Taifa.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, alisema wataalamu hao waliamua kuvunja mkataba walipoona mkandarasi wa kwanza hajafikisha viwango walivyotarajia na wakaamua kuwatumia wataalam wa ndani (force account) chini ya usimamizi wa RUWASA.
Mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba 2023 na utahudumia wananchi zaidi ya 20,000 wa miji ya Itumba na Isongole wilayani humo.
Mapema, Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Ileje, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji wa mradi wa maji wa Itumba-Isongole ambao utaondoa kabisa tatizo la hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 100 wilayani Ileje na kuwa na ziada ya maji.
Naye, Meneja wa RUWASA, Mkoa wa Songwe, Mhandisi Charles Pambe alisema kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita 500,000 kila moja.
Alizitaja kazi nyingine kuwa ni ujenzi wa miundombinu ya maji (treatment plant), ununuzi, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba kuu na bomba la kugawa maji (gravity main & distribution network) la umbali wa km. 78.72. Pia alisema wanatarajia kujenga chanzo kipya (intake) kwenye mto Itumba.