Na WAF – DAR ES SALAM
Mpango Mpya wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) umezinduliwa leo rasmi ambapo umekabidhiwa dhamana ya kutokomeza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi Nchini.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezindua mpango huo leo Novemba 23, 2023 Jijini Dar es salaam ambapo amesema licha ya mafanikio ya iliyokuwa Mpango taifa wa kuzibiti Ukimwi lakin bado kuna changamoto ya maambikizi mapya.
“Bado tuna kazi ya kufanya hususani kupunguza na kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24 na pia kutokomeza maambukizi mapya ya kutoka kwa mama kwenda kwa Mtoto, haiwezekani katika karne hii kwa kweli pamoja na wataalam tulionao, Rasilimali, dawa tushindwe kuitokomeza hii hali”. Amesema Waziri Ummy.
Pia amesisitiza NASHCoP kwa kushirikiana na jamii kuendelea kuhimizana na kuhimiza makundi yaliyo katika hatari zaidi kama vile wasichana na wavulana walio katika rika balehe kuzingatia huduma jumuishi.
“Wanawake na vijana, akinamama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto wao kwenda kupata huduma Jumuishi. Wataalamu wetu na jamii inayotuzunguka kufuatilia kutoa huduma hizo kwa weledi kulingana na miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya”. amesema Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amegusia suala la Magonjwa yasiyo ambukizwa na kusisitiza jamii kuchukha tahari juu ya magonjwa hayo yatokanayo mtindo maisha na chakula.
“Huu ndio ukweli ukiwa na UKIMWI na ukazingatia dawa unaishi vizuri kuliko ukiwa na sukari au presha ya damu, tuogope magonjwa yasiyo ya kuambukiza na tuwe na tahadhari nayo”. Amesema Waziri Ummy.