* Walipewa sh. bilioni 2, walumbana ya zaidi ya miezi 16
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje waache malumbano na badala yake wafanye kazi kwa pamoja.
“Tumeleta fedha sh. bilioni 2 za ujenzi wa jengo la Halmashauri tangu mwaka jana lakini ninyi bado mnabishana mjenge wapi jengo hilo. Au mnataka nizirudishe hizo fedha?” alihoji na kujibiwa hapana.
“Tumeleta fedha mjenge jengo jipya lakini ninyi mnataka mbomoe lililopo ili mjenge jingine wakati hapo hakuna eneo la kutosha kupanua mji wenu. Serikali imegoma msibomoe hayo majengo, na badala yake mnatakiwa mwende kujenga eneo la nyumba 10,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Alhamisi, Novemba 23, 2023) wakati akizungumza na watumishi, wakuu wa idara, viongozi na wakuu wa taasisi walioko wilayani Ileje kwenye kikao cha watumishi kilichofanyika katika ukumbi wa RM, Ileje, mkoani Songwe.
Alisema madiwani wana nguvu zote kwenye Halmashauri lakini ni lazima pia wasikilize ushauri unaotolewa na watalamu. Baraza la Madiwani lilikuwa linalumbana na watumishi juu ya kujenga ofisi za Halmashauri hiyo eneo la Itumba (walipo sasa) ambalo ni dogo na wakatoa wazo la kutaka kubomoa majengo yaliyopo ili wajenge mapya.
Maeneo yaliyokuwa yanasababisha mvutano ni Ipapa ambalo lilipendekezwa na watumishi kwa vile ni kubwa na litaweka majengo mengi ilhali madiwani walitaka lijengwe eneo la Nyumba 10 kwani tayari palishajengwa ukumbi wa Halmashauri.
Waziri Mkuu aliwataka watumishi hao wabainishe vyanzo vingine vya mapato ili kupanua wigo wa ukusanyaji mapato wilayani humo na kwamba sh. bilioni 1.9 wanazokusanya kwa mwaka, hazitoshelezi mahitaji. “Watumishi wa Halmashauri kila mmoja ashiriki kubainisha vyanzo vingine vya mapato kwenye eneo lake la kazi. Na heshima ya diwani ni kuona kata yake inachangia mapato kwenye Halmashauri yake,” alisema.
Mapema, Waziri Mkuu alikwenda kukagua hatua iliyofikiwa kwenye ukamilishaji wa miundombinu ya hospitali ya wilaya ya Ileje na baadaye kuzungumza na wananchi kwenye stendi ya Itumba, wilayani humo.
Akitoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na Wabunge wa mkoa huo, Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi waliokuwa wanamsikiliza kwamba jukumu la ujenzi wa uzio kwenye hospitali yao ya wilaya ni la Halmashauri kwani wanapaswa kuonesha fedha ilyokusanywa imechangia kitu gani kwenye wilaya hiyo.
“Nimeenda kukagua wodi ya wanawake na pia wodi ya wanaume. Wodi hizi ziko umbali wa mita 10 kutoka kwenye makazi ya watu. Tengenezeni nguzo, tafuteni wavu mpige fence ili kulinda eneo la hospitali.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Mbozi ambako atakagua ujenzi wa barabara ya Ruanda -Nyimbili – Izyila- Itumba yenye urefu wa km.76.69 kwa kiwango cha lami, atakagua mradi wa usambazaji wa umeme REA III – II katika kijiji cha Ivugula na kuwasha umeme. Pia ataweka jiwe la msingi kwenye ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Songwe.