Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Katibu tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta ametoa wito kwa Walimu wa msingi wa somo la Kiingereza (English) ,kusambaza ujuzi wa somo hilo kwa walimu wenzao katika kipindi hiki ambacho Serikali inatarajia kutekeleza mtaala mpya ifikapo Januari 2024.
Mchatta ametoa wito huo, wakati alipofungua mafunzo ya kusimamia na kutekeleza muundo wa somo la kiingereza kwa shule za msingi kulingana na Mtaala mpya wa Elimu ya Msingi unaotarajiwa kuanza kutekelezwa Januari 2024.
Amesema, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na OR TAMISEMI kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania chini ya ufadhili wa Shirika la la Uingereza (UKAID) kupitia mradi wa “Shule Bora” imeandaa mafunzo endelevu ya Walimu kazini (MEWAKA) kuhusu Muhtasari wa Somo la Kiingereza kulingana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika mitaala mipya.
Aidha, Mchatta amesema, lengo la mafunzo haya ni kukuza uwezo wa walimu wa somo la Kiingereza wa shule za Msingi kutekeleza Mtaala Mpya, kuimarisha umahiri wa washiriki katika kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Kiingereza ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi wote.
Nae Ofisa Elimu Mkoa wa Pwani ,Sara Mlaki amesema, kupitia mafunzo haya kwa Walimu wa Msingi wa somo la kiingereza katika Wilaya ya Chalinze yataenda kuleta mabadiliko chanya katika ufundishaji na ujifunzaji na kuongeza ufaulu hasa katika somo la kiingereza.
Mlaki amesisitiza walimu kupeleka ujuzi walioupata kwa walimu wengine ili iwe chachu ya kuongeza ufaulu katika Wilaya ya Chalinze hasa katika somo la kiingereza (English).