……………..,………
Na Mwandishi wetu.
Tanzania ni miongoni mwa Mataifa zaidi ya 190 yanayoshiriki mkutano wa 24 wa Kimataifa wa Nchi zenye vivutio vya Urithi wa Dunia, unaofanyika Paris nchini Ufaransa kwa siku mbili.
Akishiriki Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba amebainisha kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na maeneo mengi yaliyo kwenye orodha ya Urithi wa Dunia, ambayo ni alama ya Taifa na chanzo muhimu cha vivutio vya Utalii wetu hivyo ushiriki wake katika Mkutano huo utakuwa chachu ya Uhifadhi na Utalii nchini.
Ameongeza kuwa Tanzania ina vivutio saba muhimu vilivyoingizwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Ngorongoro, Mji Mkongwe wa Zanzibar (Stonetown), Pori la Akiba Selous, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songomnara na Michoro ya Miambani Kondoa, hali inayoifanya Tanzania kujulikama Kimataifa pia kuwa miongoni mwa nchi chache Barani Afrika zenye vivutio kama hivyo.
Aidha ameongeza kuwa kuendelea kubaki kwa maeneo hayo katika orodha ya Urithi wa Dunia ni matokeo chanya ya uongozi bora na wenye kujali Uhifadhi na kutangaza utalii chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kamishna Wakulyamba ametoa rai kwa Watanzania kuunga mkono juhudi za Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kushiriki kuhifadhi maliasili kwa faida ya kizazi kilichopo na vizazi vijavyo.
Akizungumzia Mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo Kale nchini Dkt. Christowaja Ntandu amebainisha kuwa pamoja na agenda zingine, Mkutano huu utachagua wajumbe wa kamati ya Urithi wa Dunia na Tanzania imepata bahati ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa kusimamia uchaguzi huo.
Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki mkutano huo umejumuisha Wajumbe kutoka TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Tume ya Taifa ya UNESCO ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Bi. Fatuma Mabrouk Khamis.