Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas (wa pili kulia), akipokea sehemu ya mizinga 200 ya kufugia nyuki kwa ajili ya vikundi vya ufugaji vya wilaya za Gairo na Kilombero, kutoka kwa Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao, wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Programu ya ugawaji mizinga hiyo kwa wafugaji wa mikoa ya Morogoro, Tabora na Njombe. Uzinduzi huo ulifanyika katika msitu wa Msingisi uliopo eneo la Kijiji cha Msingisi, wilayani Gairo. Wa pili kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango na kulia Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas (kulia), akimkabidhi moja kati ya mizinga ya nyuki iliyotolewa na Benki ya NMB kwa mwakilishi wa kikundi cha Juhudi Msingisi, Naomi Mbuhe, wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Programu ya ugawaji mizinga hiyo kwa wafugaji wa mikoa ya Morogoro, Tabora na Njombe. Wa pili kulia ni Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao.
…………………………
Benki ya NMB imezindua Programu Endelevu ya Ugawaji Mizinga ya Nyuki 500 kwa vikundi 17 vyenye wafugaji zaidi ya 300, katika mikoa ya Morogoro, Tabora na Njombe kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu Tanzania (TFS).
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa program hiyo uliyofanyika katika msitu wa Msingisi – Gairo, Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao amesema kuwa, NMB imewezesha kutengeneza mizinga 500 ya kisasa kwa ajili ya kuwagawia wafugaji nyuki katika mikoa ya Morogoro, Tabora na Njombe, Lakini pia benki hiyo imetenga Sh. Milioni 41i kwa ajili ya kuwezesha mafunzo kwa wanufaika wa mizinga hiyo katika mradi wa kusapoti ufugaji wa nyuki.
“Nyuki ili wazaliane ni lazima misitu ilindwe na moja ya sababu ya NMB kutoa mizinga hii 500 ni juhudi za kulinda misitu yetu ikienda sambamba na upandaji miti ambapo mpaka sasa miti 750,000 tayari imepandwa nchini kwa kushirikiana na TFS na wananchi wanapata mazao ya misitu kwa kutunza mazingira.” amesema Shao.
Bw. Shao alieleza zaidi kuwa katika mgao wa mizinga hiyo 500 Mkoa wa Morogoro umepata mizinga 200, Tabora 200 na Njombe 100 na kupitia NMB Foundation watatoa elimu kwa vikundi 17 vya ufugaji nyuki juu ya ufugaji nyuki wa kisasa, fedha na uvunaji wa asali ili asali itayovunwa iwe ya ubora wa kiwango cha juu cha kuuzwa nje ya nchi.
Mgeni rasmi katika shughuli hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii – Dk. Hassan Abbas aliipongeza Benki ya NMB kwa kuja na programu hii ambayo pia inasapoti Serikali katika kuipa thamani zaidi Kampeni ya Achia Shoka, Kamata Mzinga na hivi karibuni, Serikali imeiinginza sekta ya asali na nyuki katika Programu ya Kujenga Kesho Iliyo Bora kwa Vijana na Wanawake nchini (BBT).
Lakini pia, juhudi hizi ni sehemu ya maandalizi ya Serkali kuelekea Mkutano Mkuu wa Wafugaji Nyuki Duniani utakaofanyika Tanzania mwaka 2027, ambao utawahusisha waataalum wakimataifa zaidi ya 4000.
Dkt. Abbas alisisitiza kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uzalishaji wa mazao ya nyuki yenye kiwango cha juu cha ubora kutokana na uwepo wa misitu yenye mimea inayotoa chakula kwa nyuki huku sekta hiyo ikichangia ajira zaidi ya ajira ya watu milioni mbili na kukadiliwa kuwa na uwezo wa uzalishaji wa asali tani 138,000 kwa mwaka.
Kamishna wa Uhifadi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) TFS, Profesa Dos Santos Silayo amesema Benki ya NMB imekuwa na ushirikiano nao katika utunzaji mazingira na upandaji miti tangu mwaka 2022 kupitia kampeni yao ya Miti Milioni na anawashukuru sana.