Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania-TPA, inakusudia kujenga matanki yake kwa ajili ya kuhifadhi nishati ya mafuta ili kuondoa ucheleweshaji wa meli za mafuta katika Bandari ya Dar es salaam.
Hii ni kwa mujibu wa Meneja wa Kituo cha kupakulia mafuta Mhandisi Yona Malago wakati akitoa ufafanuzi leo kwa waandishi wa Habari waliotembelea Bandari ya Dar es salaam.
Mhandisi Malago, amesema tayari Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa matanki hayo ameshapatika baada ya serikali kutenga kiasi cha fedha katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2023/2024.
“Nikuambieni tu kuwa sasa hivi serikali haina matanki ya kuhifadhi mafuta na kinachofanyika tunategemea matanki ya watu binafsi, hivyo tukijenga matanki yetu tutaondokana na hali ya ucheleweshaji wa meli za mafuta bansarini, alisema Malago”
Naye, Abasi Msukulu, amesema meli kubwa za mafuta yanayoingizwa nchini huchukua kati ya siku tatu hadi nane kushusha mafuta kulingana na wapokeaji wa mafuta wanavyopokea.
Amewaambia waandishi wa habari waliotembelea boya maalumu la kushusha mafuta aina ya Disel lililopo eneo la kisinda mji mwema, kuwa uwekezaji uliofanywa na serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, umesaidia meli kubwa za mafuta zaidi ya tani elfu 50 hadi laki moja kushushwa katika boya hilo lililopo kwenye kina kirefu cha maji ya bahari ya Hindi.
Katika hatua nyingine, Maboresho yanayoendelea kufanyika katika Bandari ya Dar es salaam yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa malalamiko ya wananchi hususu wizi wa baadhi ya vifaa vya magari katika Bandari hiyo muhimu inayotumiwa na mataifa mbalimbali katika ukanda wa Afrika.
Afisa Utekelezaji Msaidizi Bandari ya Dar es salaam, Aman Kimario amesema hayo leo katika ziara ya waandishi wa habari kutoka Uhuru Fm na baadhi ya vyombo vingine ili kujionesha maboresho katika Bandari ya Dar es salaam.
Amesema kwa sasa magari zaidi ya elfu moja na mia tano yanapakuliwa kutoka katika meli kwa saa nane kwa siku, hii ikitokana na uboreshaji wa kuongeza gati maalumu namba ziro kwa ajili ya magari.
“Kwenye gati hii namba ziro ambayo ina eneo lake maalumu ambalo zaidi ya magari elfu tatu yanauwezo wa kupaki kwa wakati mmoja, na imesaidia sana utendaji kazi katika bandari yetu hii ya Dar es salaam”
” Na kama mteja akikamilisha taratibu zake zote za forodha anaweza kuondoka na gari yake ndani ya siku” alisema Kimario.
Kwa mujibu wa Kimario, udokozi wa vifaa vya magari kwa sasa haupo hii ni kutokana na mifumo mizuri waliyoiweka ikiwa ni pamoja na kuongeza kamera katika eneo hilo la gati namba ziro.
“Kwa sasa ukisikia kuna gari vifaa vyake havionekani jua kabisa gari hilo vifaa hivyo vimepotea huko huko lilipotoka na sio hapa kwenye Bandari yetu ya Dar es salaam” alisema Kimario.
Wakati huo huo, Zaidi ya Tani Elfu Moja na mia tano za mizigo mchanganyiko kwa siku hupakukiwa kutoka katika Meli mbalimbali zinazotia nanga katika bandari ya Dar es salaam.
Hayo yamesemwa leo na Afisa Mwandamizi Kitengo cha Mizigo Mchanganyiko, Juma Juma wakati akitoa ufafanuzi wa waandishi wa Habari wa Uhuru FM na baadhi ya vyombo vya habari vikivyotembelea Bandari ya Dar es salaam kujionesha shughuli mbalimbali za bandari hiyo.
Juma, amesema hali ya hewa ikiwa mbaya kwa maana ya kuwepo kwa mvua husababisha changamoto ya ushushaji wa mizigo mchanganyiko, hivyo kusababisha mizigo kuchukua muda mrefu kupakuliwa kutoka kwenye meli.