Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Novemba 20
UTEKELEZAJI wa kufundisha somo la kiingereza (English)kuanzia darasa la kwanza kufuatia mabadiliko ya mtaala wa elimu ya Msingi 2023 utaanza rasmi January mwaka 2024 .
Utekelezaji huo ni hatua itakayomuandaa mwanafunzi kujiimarisha kwenye matamshi na kufanya mawasiliano vizuri kwa lugha Kiingereza kuanzia ngazi chini ya msingi.
Somo hilo litaanza kufundishwa darasa la kwanza badala ya darasa la tatu tofauti na ilivyokuwa mtaala wa elimu ya Msingi wa mwaka 2016.
Mwenyekiti wa Maandalizi ya mafunzo ya somo la Kiingereza (English) ,kutoka Chuo Kikuu Prof.Gastor Mapunda , aliyaeleza hayo katika mafunzo yaliyoandaliwa kwa kushirikiana baina ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ,Wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania katika programu ya Mradi wa Shule Bora ambayo inatekelezwa katika mikoa Tisa, Tanzania Bara kwa Ufadhili wa Shirika la msaada la Uingereza (UKaid) na kwa usimamizi wa Cambridge Education, kwa viongozi wa elimu Halmashauri ya Chalinze, Mkoani Pwani.
Aliwaasa ,walimu wa somo la kiingereza waongeze umahiri wa kutosha ili kuleta matokeo chanya katika utekelezaji huo .
Vilevile Prof.Mapunda aliwataka maofisa elimu ,wadhibiti ubora wayatambue maboresho hayo na kwenda kuyasimamia kikamilifu.
“Kwa mujibu wa mtaala utaanza kwa awali ,darasa la kwanza na la tatu ,lengo la kufanya mabadiliko hayo ni kutekeleza ahadi aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2014 na madadiliko ya mtaala ili kuwa na sera na mitaala inayoakisi mahitaji ya sasa na baadae”
“Katika kuzingatia maono ya Rais kwenye mabadiliko haya tunataka kumuandaa mtoto aweze kufikia ndoto zake “alifafanua Prof Mapunda.
Awali Mkuza Mtaala wa somo la Kiingereza kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET ), Neema Matingo alieleza mafunzo hayo yanalenga kuwapa uelewa mpana viongozi wa elimu kuhusu mabadiliko ya mtaala huo.
“Baada ya mafunzo haya yatafuata mafunzo ya siku tano kwa ajili ya walimu mahiri wa somo la English katika halmashauri ya Chalinze kuanzia Novemba 21hadi 25 yanayoshirikisha wawezeshaji kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, chuo cha Aghakhan, chuo cha ualimu Vikindu,sanjali na mdhibiti ubora wa Kanda”.
Kwa upande wake ,Hawa Waziri Mwalimu wa somo la Kiingereza kutoka shule ya Msingi Magome ,Kata ya Pera ,Chalinze alieleza, mafunzo hayo yatawaweka vizuri, kuzidisha ari na ufanisi .
Alieleza, wanaamini baada ya mafunzo wataweza kuchambua muhtasari wa somo la Kiingereza kwa darasa la kwanza na la tatu ,kuandaa na kutumia mbinu za ufundishaji wa somo hilo.
Msimamizi wa elimu kata ya Lugoba ,Rashid Masimba yeye alipongeza mradi wa Shule Bora na Taasisi ya Elimu Tanzania kuona umuhimu wa kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya mtaala huo kwa walimu wa somo husika,walimu wakuu na viongozi wa elimu.
Mafunzo hayo yatashirikisha viongozi wa elimu 42 ,walimu 100 kutoka katika shule teule za wilaya ya Chalinze na Kisarawe ,lengo likiwa kukuza uwezo wa walimu wa somo la Kiingereza wa Shule za Msingi kutekeleza mtaala mpya wa mwaka 2023.