Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amefanikiwa kutuliza hasira za wananchi wa kijiji cha Msanda Muungano wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa waliolazimika kuusimamisha msafara wake ili awasikilize na kutatua mgogoro wa ardhi wa muda mrefu.
Wakazi hao waliojazibika walisimamisha msafara huo ambao ulikuwa unaelekea kijiji cha Sikaungu uliokuwa unaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere kuekea kwenye mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wananchi na Shirika la Efatha Ministry.
Waziri Silaa alisimama na kuwasikiliza wakazi hao ambapo aliwaahidi kuleta kamati maalumu ya kushughulikia migogoro ya ardhi ya eneo hilo lote ambayo itajumuisha wataalamu wa Ardhi kutoka Makao Makuu Dodoma, Mkoa wa Rukwa, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wawakilishi wa wananchi.
Kamati hiyo imepewa siku sita tu za kukamilisha taarifa yake ambapo Waziri Silaa mwenyewe ameahidi kuja kuiwasilisha na kumaliza mgogoro huo tarehe 24 Novemba 2023.
Mgogoro huo wa muda mrefu umekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa amani na kupelekea mauaji ya kila mara jambo ambalo limelazimu wakazi hao kuomba Mhe. Silaa kuutatua mgogoro huo kwa haraka ili usiendelee kuleta madhala.