Kamishna wa idara ya uendelezaji sekta ya fedha ,Dkt Charles Mwamwaja akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonyesho ya tatu ya wiki ya huduma za fedha kitaifa yanayoanza kesho mkoani Arusha.
……….
Julieth Laizer, Arusha.
Arusha.Waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ,Kassimu Majaliwa Kassimu anatarajiwa kufungua maonyesho ya tatu ya wiki ya huduma za fedha kitaifa novemba 22, yatakayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha .
Akizungumzia kuhusiana na maonyesho hayo yanayoanza kesho novemba 20 yatakayohudhuriwa na taasisi mbalimbali za kifedha ,Kamishna wa idara ya uendelezaji sekta ya fedha Dkt. Charles Mwamwaja amesema serikali imekua ikitoa mwongozo katika kuwawezesha utoaji wa huduma za kifedha nchini ,katika programu ya uelimishaji wa umma huku yakilenga utoaji wa elimu kwa wananchi .
Dkt Mwamwaja amesema takwimu zinaonyesha idadi kubwa ya watanzania Bado hawajafikiwa na taasisi za kifedha, ambapo asilimia 53.8 tu ndiyo waliofikiwa na huduma hizo.
Amesema wamekusudia kufikisha lengo la asilimia 80 ya watanzania kuwakutanisha na huduma rasmi za kifedha , huduma za masoko ya umma,mitaji,na mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
“baadhi ya wananchi bado wanatumia njia isiyo sahihi ya utunzaji wa fedha zao ikiwemo kuhifadhi ndani,kuweka kwenye vihenge na wengine kuchimbia chini hali ambayo amesema wananchi watapata elimu rasmi ili kuepuka njia hizo”.amesema Dkt Mwamwaja.
Aidha wizara ya Fedha ndiyo iliyoratibu maonyesho hayo kwa ushirikiano wa wadau wengine wa fedha wakiwemo benki kuu ya Tanzania huku Meneja msaidizi wa mawasiliano kutoka Benki kuu ya Tanzania , Noves Mosses ,amesema benki hiyo ikiwa ni ya serikali na msimamizi wa taasisi zingine za kifedha , imejikita kutoa elimu kwa wananchi ili kuwa na uelewa mpana ,na kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.
Ametoa wito kwa wananchi wenye changamoto ama kuhitaji kupata ufafanuzi kuhusu masuala ya kifedha kufika uwanjani mapema kupata elimu hiyo.
Kwa upande wake Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika kutoka tume ya maendeleo ya ushirika ,Grace Msambaji amesema vyama vya ushirika humwinua mnyonge kutoka chini jambo ambalo amesema wamejipanga kuwahudumia wananchi katika kuendeleza uchumi wa watanzania.
Aidha kauli mbiu ya maonyesho hayo ni elimu ya Fedha ,msingi wa maendeleo ya kiuchumi.