Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAZIRI wa Madini, Anthony Peter Mavunde, ameipongeza kampuni ya Franone Mining LTD, inayomiliki kitalu C kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite, Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa namna inavyosaidia jamii inayowazunguka.
Hata hivyo, Waziri Mavunde, amewataka wawekezaji wa madini nchini kuwa na ushirikiano na jamii inayowazunguka ili waweze kufanya shughuli zao za uchimbaji kwa amani na ushirikiano.
Waziri Mavunde ameyasema hayo baada ya kutembelea mgodi wa Franone na kukutana na wanawake waliopata ajira kupitia kampuni hiyo walioajiriwa kusuka kamba na wengine kupewa mchanga na kuchekecha ili kupata mabaki ya madini hayo.
Amesema wawekezaji wa maeneo mengine ya madini wawe na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka kwani ametembelea baadhi ya maeneo ya madini na kukutana na msuguano wa wawekezaji na jamii inayowazunguka.
“Nichukue fursa hii kumpongeza mmiliki wa Franone Mining LTD, Onesmo Mbise kwa ushirikiano mkubwa alionao na jamii na sisi kama serikali tutaendelea kukuunga mkono ili usaidie jamii zaidi,” amesema.
Amewataka wanawake wanaochekecha mchanga wa madini ya Tanzanite wanaopatiwa na kampuni hiyo, kuendeleza ushirikiano katika kufanya shughuli hizo za kila siku kwa amani na upendo.
“Nia ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha jamii inanufaika na rasilimali zinazowazunguka na siyo hapa Mirerani pekee, ila ni kila maeneo yenye madini tunayasisitiza hayo,” amesema.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema hivi karibuni kampuni ya Franone Mining Ltd, ilitengeneza barabara ya kupanda migodini inayotumiwa na wachimbaji tofauti.
“Kampuni hiyo ilitengeneza barabara ya kilomita nane kwa kiwango cha changarawe hivyo kurahisisha wanaoendesha pikipiki na magari kupita kwa urahisi hasa kipindi hiki cha mvua,” amesema Sendiga.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema kampuni ya Franone Mining Ltd imekuwa ikijitoa katika kusaidia jamii inayowazunguka hasa wanawake.
“Hivi karibuni kabla ya mvua kunyesha kulikuwa na ukame kwenye kata ya Naisinyai, kampuni hii ilisaidia jamii kwa kutoa chakula kwa wanafunzi wa shule mbili za msingi,” amesema Ole Sendeka.
Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Mnyawi amesema wadau wa madini wanapaswa kutoa kiasi kidogo wanachopata kwa kusaidia jamii (CSR) kwani eneo hilo lina changamoto kubwa hasa miundombinu ya elimu.
“Wadau wa madini ya Tanzanite saidieni ujenzi wa miundombinu ya elimu, kwani unakuta shule moja ya msingi ina zaidi ya watoto 1,000 tusiiachie serikali yenyewe haitakuwa vyema,” amesema Salome.