Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Serikali itaendelea kulinda kwa nguvu na gharama zote uhuru wa wananchi wa kutoa mawazo, imani na uchaguzi katika dini, hivyo itahakikisha kunakuwa na amani na utulivu ili uhuru huo wa kuabudu na kutoa mawazo uwepo muda wote.
Dkt.Biteko amesema hayo tarehe 19 Novemba, 2023 wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za kumpongeza Mhasham Askofu Mkuu Mstaafu Paul Ruzoka na kumpokea rasmi Askofu Mkuu Mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa. Sherehe zilizofanyika katika Jimbo Kuu Kanisa Katoliki Tabora.
“Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan muda wote amekuwa akisisitiza haki kwa wananchi wote, na ili kuishi katika misingi ya utangamano haki lazima itawale. Rais anataka wananchi wasikilizwe; tunaweza kutofautiana katika maoni na mitazamo lakini kamwe tusivunje umoja wa kitaifa, tuwaunganishe watanzania na tupambane kuwaondoa wananchi katika umaskini na kuwaletea nafuu kubwa ya maisha.” Amesema Dkt.Biteko
Dkt. Biteko amesema kuwa, Mheshimiwa Rais, msisitizo wake ni kupeleka maendeleo kwa wananchi wote bila kuangalia tofauti zao, ikiwemo maji, barabara, umeme, shule na pia lengo lake ni kuendelea kuwaunganisha wananchi ili kuleta umoja nchini.
Vilevile, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt.Samia yupo tayari muda wote kushirikiana na taasisi za kidini nchini kuwaletea maendeleo wananchi.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali itaendelea kuhubiri haki na maridhiano kama msingi wa amani wa nchi na pia itaendelea kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo kwani bila kazi hakuna Taifa.
Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko amesema kuwa, Rais ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Askofu Mkuu Mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa kama ambavyo amekuwa akitoa ushirikiano kwa mtangulizi wake Mhasham Askofu Mkuu Mstaafu Paul R. Ruzoka.
Kwa upande wa Askofu Mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa na Mhasham Askofu Mkuu Mstaafu Paul R. Ruzoka wameshukuru kwa ushirikiano ambao Serikali imeendelea kuutoa kwao na wameahidi kutoa pia ushirikiano kwa Serikali.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian na Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamis Kigwangala. Pia walihudhuria Viongozi mbalimbali wa Madhehebu ya Dini kutoka ndani na nje ya nchi, na Waumini wa Kanisa Katoliki kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Tabora.