Na Beatus Maganja
Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe.Joshua Nassari amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imekuwa nguzo na mchango mkubwa katika mapato ya wilaya yake kutokana na fedha zinazotokana na shughuli za Utalii zinazofanywa na taasisi hiyo wilayani humo.
Ameyasema hayo Novemba 17, 2023 katika ziara ya kuelezea namna Serikali inavyorejesha kwa jamii kupitia shughuli za utalii, ziara iliyofanywa na TAWA Wilayani humo.
“Sehemu kubwa ya mapato tunayoyapata kwa maana ya fedha za ndani, ukiondoa mgao tunaoupata kutoka TAWA tutachechemea, tutashindwa kupiga hatua” amesema
“Hii robo iliyopita tumepata barua kutoka kwa Mkuu wa Mkoa ambayo imetupongeza kwasababu tumevuka lengo la makusanyo ambayo tulikuwa tumejiwekea, lakini kilichotufanya tuvuke ni fedha kwa ule mgao wetu kutokana na shughuli za Utalii ambazo moja kwa moja huwa zinakusanywa na TAWA na baadae tunarudishiwa asilimia yetu” ameongeza
Aidha Mhe. Nassari amesema faida zitokanazo na shughuli mbalimbali za utalii zinazofanywa na TAWA wilayani humo zimeisaidia wilaya yake kuweza kuwahudumia wananchi kikamilifu kwa kujenga vituo vya afya na zahanati, kununua vifaa tiba, kujenga vyoo kwenye mashule na miradi mingine mingi ya maendeleo.
“Kutokana na faida zote hizo niseme wazi kabisa bila kupepesa macho kwamba Kwa wilaya ya Monduli TAWA ni mdau wetu namba moja” amesisitiza Mhe. Nassari
Wananchi waishio wilayani humo, wameeleza kuridhishwa na utendaji mzuri wa TAWA na kufurahia faida zitokanazo na shughuli za Utalii zinazofanywa na taasisi hiyo na hivyo kuahidi kushirikiana nao katika shughuli za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali Wanyamapori kwa ujumla.
“Tunashukuru jitihada Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TAWA ametuwezesha kuchangia miradi ya maendeleo kama Jengo la watumishi tumejenga kwa hela la TAWA, Jengo la wodi ya wagonjwa, Jengo la ofisi ya Kijiji vyote tumejenga kwa fedha za TAWA ” amesema Bi Teresia Silaa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nafco
“Mwanzo wananchi walikuwa hawaelewi umuhimu wa hifadhi lakini kwasasa wananchi wetu wameelewa sana faida za uhifadhi, kwahiyo tunashukuru sana” ameongeza Mtendaji huyo