Na Sophia Kingimali
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Wanawake Jinsi na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema wizara imeanza kutekeleza miongozo ya ushirikiano na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kuhakikisha ajenda ya jinsia inatekelezwa katika sekta zote.
Hayo ameyasema Novemba 17,2023 jijini Dar es salaam wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa mawaziri wa fedha na jinsia wenye lengo la kujadili kuhusu uwekezaji kwa maendeleo ya usawa wa jinsia ambao nchi 22 zimehudhuria mkutano huo.
Amesema katika mkutano huo wametoka na maazimio matano yote yakiwa na lengo la kusukuma mbele ajenda ya jinsia na kuwa na usawa wa kisera kwa nchi zote za Afrika.
“Lazima kuwa na jicho la ufuatiliaji ili kujua fedha zilizopagwa je zimetumika katika kuendeleza ajenda au la kwani lengo ni kuendeleza ajenda na kuhakikisha kuna maendeleo yenye usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake”amesema Gwajima.
Akisoma maadhimio ya mkutano huo amesema moja ya maadhimio yao ni kutizama swala la ukatili wa jinsia ili liweze kuwekewa bajeti kwa ajili ya kupambana nalo.
Ameongeza kuwa pia wamedhamiria kuboresha teknolojia na ubunifu kuelekea usawa wa kijinsia na maendeleo ya wanawake lakini pia kumuwezesha na kumpa elimu mwanamke.
Ameongeza pia kuwa nchi zimeendelea kuwa na amani kwa sababu wanawake wameshiriki katika kuhakisha amani na utulivu wa nchi unapatikana.
Sambamba na hayo Dkt. Gwajima amesema mwanamke anapaswa kuwa na kasi kama mwanaume kwenye maendeleo ili wote waweze kuwa na mchango sawa kwa nchi.
Aidha ameongeza kuwa wanawawake wamekuwa wakifanya shughuli nyingi za kimaendeleo lakini hazijarahisishwa wala kupewa dhana za kisasa za kufanyia shughuli zao majumbani.
“Kwa Tanzania wanawake wengi ndiyo wapo katika kilimo na wanazalisha kweli kweli kazi yao ni asilimia 80 lakini hawana nyenzo za kufanyia kazi zao lakini bado kuna ukatili wa kijinsia unaowaandama na kushindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi”amesema
Kwa upande wa mkurungenzi wa UN WOMEN Kanda ya Afrika mashariki Dkt. Maxime Houinato amesema mgawanyo wa haki za wanawake ni chachu ya kukuza uzalishaji na maendeleo katika mataifa.
“Katika kufikia malengo swala la jinsia linahitajika kuwekewa makazo katika sera na bajeti ili uchumi wa mwanamke uweze kukua kwani uchumi wa mwanamke ukikua na mataifa nayo yanakua”amesema Dkt Houinato.