Na Beatus Maganja
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewajengea walimu wa shule ya msingi mangara iliyopo kata ya Mangara wilayani Babati Mkoa wa Manyara nyumba moja ya Kisasa yenye uwezo wa kuwahudumia walimu wawili “Two in One”
Nyumba hiyo ambayo Kila upande ina jumla ya vyumba vitatu vya kulala, sebule moja, stoo, jiko choo na bafu imejengwa kutokana na gawio la fedha zitokanazo na shughuli za Utalii zinazofanywa na TAWA wilayani humo.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Magara Bi Mwendaeli Mbwambo ameishukuru Serikali kwa msaada wa nyumba hiyo na kudai umeongeza morali ya walimu hao kufanya kazi kwa bidii.
“Kwa asilimia kubwa napenda kuwapongeza TAWA kwa ajili ya mambo yote waliyoyafanya, wametujengea nyumba ya walimu “Two in One” ambayo wanaishi walimu wawili, Kwakweli walimu wanafurahi sana” amesema
“Pia wametujengea madarasa na ofisi ambapo pia kulingana na wingi wa wanafunzi tulionao itasaidia kupunguza wanafunzi kwenda shule “B”” ameongeza Mwalimu huyo
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Magara Bw. Ramadhani Nyonyi amesema tangu fedha hizo zinazotokana na shughuli za utalii zianze kuingia katika Kijiji hicho wamepata mageuzi makubwa kwenye vijiji kumi ambavyo vipo katika Jumuiya ya hifadhi ya Wanyamapori Burunge
“Fedha hizi zimefanya miradi mingi ambayo inaisaidia jamii kwenye Kijiji hichi kufurahi na kuwa hivi” amesema
“Kwa upande wa sekta ya elimu fedha hizi zimetusaidia kumaliza madarasa sita na ofisi tatu pia tuna mpango wa kuanza kuchimba choo” ameongeza Mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Mangara
TAWA inaendelea kuwakumbusha wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi nchini kuendelea kuzingatia sheria ya uhifadhi kwa kuachana na vitendo vya uvunjifu wa sheria hiyo kwa kulima, kuchunga mifugo na kuanzisha makazi ndani hifadhi pamoja na ujangili wa aina yoyote Ile kwani vitendo hivyo vinaleta athari kubwa katika shughuli za Utalii ambazo ni chanzo kikubwa cha pato la Taifa ambalo pia huchangia katika miradi hiyo ya maendeleo kwa jamii.