Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam kufuatia Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Romania Mhe. Klaus Iohannis nchini Tanzania tarehe 17 Novemba 2023 .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Romania Mhe. Klaus Iohannis wakati wakishuhudia utiaji saini wa Mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo iliyotiwa saini na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Prof. Raphael T. Chibunda na Waziri wa nchi wa masuala ya Dunia na Mikakati ya Kidiplomasia wa Romania Mhe. Traian- Laurentiu Hristea kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 17 Novemba 2023.
…………………….
KATIKA kuendeleza ushirikiano wa Tanzania na Romania nchi hizo zimetia saini za makubaliano katika sekta ya kilimo, mazingira na majanga.
Hayo yamesemwa leo, Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Romania Klaus Iohannis wakati wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza mazungumzo ya ndani.
Akizungumzia ushirikiano huo, Rais Samia alisema Tanzania na Romania zimekuwa na ushirikiano mzuri, hivyo ujio wa Rais huyo nchini imeendelea kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili huku akieleza katika mazungumzo yao wamekubaliana kushirkiana katika masuala mbalimbali yakiwemo ya dawa na usindikaji kwa mazao ya kilimo.
Rais Dk.Samia amesema kwa niaba ya wananchi wa Tanzania wanayofuraha kubwa ya kumpokea Rais na ujumbe wake na kwamba wataendelea kudumisha ushirikiano, ili uweze kulete tija kwa wananchi wa nchi zao.
Dk Samia amesema uhusiano wa Tanzania na Romania ulainza Mei mwaka 1964 ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hivyo Romania ni mbia wa maendeleo kwa muda mrefu na kwamba atahakikisha mashirikiano hayo yanakuwa endelevu.
“Tumekubaliana kuendelea kuimarisha sekta mbalimbali kama sekta ya dawa, usindikaji wa mazao ya kilimo, madini, biashara, ulinzi, majanga na nyingine,” amesema.
Pia Rais Samia amesema katika mazungumzo yao wamekubaliana ufadhili wa masomo katika udaktari na famasia, eneo ambalo bado lina uhitaji mkubwa,” ameongeza.
Amesema katika mazungumzo hayo, Romania imekubali kutoa nafasi 10 za Watanzania kwenda kusoma kwa masomo ambayo watachagua, huku Tanzania ikitoa nafasi tano za ufadhilii kwa wanafunzi wa tano wa Romania kuja kusoma nchini.
“Tumezungumzia kuhusu kuimarisha sekta ya biashara hasa kukuza zaidi biashara kwa kuangalia maeneo ambayo tunaweza kufanya pamoja, kualika wafanyabiashara wa Romania kuja Tanzania na Watanzania kwenda Romania kubadilisha uzoefu.
Amesema wamekubaliana mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zao kuendelea kuzungumza mara kwa mara, ili kuhakikisha fursa zilizopo baina yao zinatumika ipasavyo kwa maslahi ya pande zote.
Aidha, Rais Dk.Samia ameipongeza Romania kukubali kuendelea kushirikiana na nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Pia amesema wameomba Romania isaidie kuwapa nguvu katika kuhakikisha Tanzania inafanikiwa katika eneo la nishati safi ambayo inahitaji kwa matumizi mbalimbali kwa sasa.
Kwa upande mwingine Rais Samia amesema wakati umefika kwa kuanza utekelezaji wa makubaliano waliyosaini mwaka 2018, kuhusu kufanya mikutano ya mazungumzo ya kisiasa.
Amesisitiza ni matumaini yote ambayo wameyazungumza yatatekelezwa kwa maslahi ya nchi zote mbili.
Naye Rais Iohannis amesema mwakani Romania na Tanzania zinatumiza miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia, hivyo kupitia ziara hiyo ya kwanza kufanywa na kiongozi wa kitaifa wamejadiliana namna ya kuboresha na kuendeleza mazuri ambayo yamefanyika.
Rais Iohannis amesema Tanzania ni moja ya nchi ambayo wamekuwa wakishirikiana kwa mafanikio makubwa na kwamba watahakikisha unaendelea.
Amesema mikakati yao ya kurejesha ushirikiano na nchi za Afrika utahakikisha Tanzania inanufaika zaidi.
Rais Iohannis amesema sekta ya kilimo na majanga itapewa msukumo mkubwa kwani zina mchango kwenye maendeleo.
“Tunatamani sekta ambazo tumekubaliana zinafanikiwa kwa kasi ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana. Mfano sekta ya ulinzi, teknolojia na usalama wa mitandaoni,”amesema.