Na Sophia Kingimali
Waziri wa afya Dkt. Ummy Mwalimu amewataka wataalam wa afya,watafiti,walimu na wataalam wanaotoa elimu ya lishe katika jamii kutoa elimu ya hiyo na kusambaza muongozo wa lishe ili kuhakikisha elimu ya lishe bora inamfikia kila mwananchi.
Wito huo ameutoa leo Novemba 16,2023 jijini Dar es salaam wakati akizindua mwongozo wa kitaifa wa chakula na ulaji hafla iliyofanyikia katika soko la kisutu na kuhudhiliwa na viongozi na wadau mbalimbali wa Afya.
Amesema mwongozo wa lishe unapaswa kumfikia kila mtu ili kubadili mtindo wa maisha na kuacha tabia bwete zinazochochea ongezeko la magonjwa yasiyoyakuambukiza kama shinikizo la damu na kisukari.
“Kuna dhana potofu kama kula mlo kamili ni gharama sio kweli makundi yote ya chakula yanapatika kwa watu wa mazingira yote bila kujali masikini au Tajiri vijijini au mjini na ndio maana tunasisitiza muongozo huu uweze kumfikia kila mwananchi lakini pia elimu iendelee kutolewa kila sehemu”amesema Ummy.
Ameongeza kuwa lishe duni ni kisababishi kikubwa cha utapiamlo wa aina zote katika jamii na kusababisha taifa kupoteza mpaka asilimia 10 ya pato ghafi bila kujumuisha madhara ya kiakili yanayopelekea kupungua kwa utayar wa kujifunza.
Amesema kutokana na takwimu za utafitia wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya maralia zinaonyesha zinaonesha kiwango cha uzito au unene uliopitiliza umeongezeka kutoka asilimia 18 mwaka 2004 mpaka kufikia asilimia 36 mwaka 2022 huku wanaume wenye uzito uliopitiliza unene ni asilimia 17.
“Takwimu hizo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na ulaji usiofaa kwani jamii nyingi za Kitanzania bado ulaji wetu unatumia vyakula vya aina moja au mbili kukamilisha mlo”amesema
Ameongeza kuwa jamii nyingi zimeacha matumizi ya vyakula vya asili visivyokobolewa ambavyo ni bora zaidi katika kuboresha hali ya lishe.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji taasisi ya chakula na lishe Dkt Germana Leyna amesema muongozo huo utasaidia kutoa hamasa kwa wananchi kutumia vyakula vinavyopatikana kwenye maeneo yao.
Amesema Tanzania imekua nchi ya 12 kati ya nchi 56 Afrika yenye miongozo ya chakula ambapo jitihada hizo zimechagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kiu kubwa ya watanzania ilikuwa ni kufahamu ale chakula kipi kwa mchanganuo upi na kwa kiasi gani sasa muongozo huu unaenda kutibu mahitaji yao”amesema Dkt. Germana.
Amesema matumizi sahihi ya mwongozo huo utasaidia kuondoa udumavu lakini kupotea kabisa kabisa kwa changamoto zinazotokana na ukosefu wa madini lakini pia kuondokana na uzito mnene.
Nae Mganga mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Dkt Rashid Mfaume ametoa pongezi kwa waziri wa kilimo kwa kuendelea kusimamia kilimo kwani kimepeleka masoko kuwa na vyakula vya kutosha.
Amesema Dar es salaam ina masoko zaidi ya 95 na kote upatikanaji wa chakula sio tatizo hali iliyopelekea kupunguza kiwango cha udumavu kwa asilimia 18.
Muongozo wa kitaifa wa chakula na ulaji umeandaliwa na taasisi ya chakula na lishe kwa kushirikiana na shirika la umoja wa mataifa la chakula na kilimo FAO unatarajiwa kusambazwa nchini kote kwa kupitia njia tofauti ikiwemo vipindi maalum kwenye vyombo vya Habari na elimu mashuleni na kwenye mikusanyiko ya watu huku serikali ikiahidi kuandaa video fupi itakayokua inaonyeshwa kwenye kila vikao vya taasisi ambavyo vitakutanisha watu zaidi ya 50.