Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Shirikisho la Wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Josephat Rweyemamu ametoa wito kwa wanachama shirikisho hilo kushiriki kwa wingi kwenye maonyesho ya wajasiliamali JUAKALI Nguvu Kazi Afrika Mashariki yatakayofanyika nchini jijini Bujumbura nchini Burundi, kuanzia Desemba 5 hadi 15 mwaka huu.
Rweyemamu ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo ambapo ameweka wazi kuwa jumuiya hiyo ilianza mwaka 1999 baada ya kurejeshwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba maonesho hayo yanafanywa kwa kuzunguka nchi wanachama.
“Maonyesho haya ni ya 23 tangu kuazishwa kwake na katika maonyesho haya zitafanyika shughuli mbalimbali, kutakuwa na siku ya Tanzanaia ambayo itafanyika Disemba 10 na itakuwa siku mahususi ya kuonyesha bidhaa zetu,”amesema
Amesema kuwa wameshatoa fomu kwa ajili ya wajasiriamali wanaotaka kushiriki wajaze na kuzirudisha mapema kwa kuzingatia muda, huku akitarajia Tanzania kuwakilishwa na washiriki 300 ambao watakuwa na bidhaa mbalimbali za kusindika, nguo na nyinginezo.
Ameongeza kuwa maonyesho hayo yanatarajiwa kuwa na wajasiriamali 1000 kutoka nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Sudan Kusini, DR Congo, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Tanzania na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuwaunganisha wajasiliamali wadogo na kati wa Afrika Mashariki kufanya biashara katika eneo la jumuiya hiyo”
Rweyemamu amesema maonyesho hayo yanafundisha wafanyabiashara namna ya kuvuka mipaka na kujua sheria na taratibu.
Mwenyekiti amesema pia wanahamasisha vijana kushiriki kwa wingi ili kuweza kuingia kwenye ujasiriamali wakiwa vijana kwa lengo la kuongeza ubunifu .
Amesema maonyesho hayo ni fursa hivyo nivema watu wakajiandikisha kwa wingi, ili kuweza kushiriki na kuweza kujifunza kwa wenzao ambao wamepiga hatua kwenye eneo hilo.
Rweyemamu amewataka washiriki kuzingatia taratibu zote za kusafiri nje ya nchi ikiwemo hati ya kusafiria, kuchanga korona, gharama za kubadilisha fedha na mengine.
Naye Mratibu Mkuu wa Maonesho hayo ya JUAKALI Nguvu Kazi, Zubeda Omar amewataka wajasiriamali kujitokeza kuchukua fomu na kwenda kushiriki na kuachana na tabia ya kulalamika kwamba hawapewi fursa.
Zubeda amesema mwitikio wa kujaza fomu za ushiriki ni mkubwa na matumaini yao ni kuona ushiriki wa Watanzania ukiwa na tija.