Kufuatia mkoa wa Njombe kuwa na hazina kubwa ya madini mbalimbali chini ya ardhi,Serikali imewataka wachimbaji wadogo wa madini wanawake mkoani Njombe kuchangamkia fursa ya uchimbaji wa madini ili waweze kujikwamua kiuchumi pamoja na familia zao.
Rai hiyo imetolewa Nerasi Mulungu ambaye ni Afisa Elimu Mkoa kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari wakati akifungua mafunzo ya mnyororo wa sekta ya madini pamoja na leseni kwa Wajasiriamali, Wadau na Wachimbaji wadogo wa madini wanawake juu ya fursa zilizopo katika sekta hiyo,
Nerasi amesema anafahamu wanawake wa mkoa wa Njombe ni wachakalikaji katika kujitafutia maendeleo ya kiuchumi, hivyo pia wanayofursa nzuri ya kugeukia uchimbaji wa madini ambao umekuwa ukisaidia kukuza uchumi.
“Lengo la kikao hiki ni kwa ajili ya kujengeana uwezo, kuelimishana kuhusu uendeshaji wa shughuli za madini kwa upande wa wanawake, hii ni fursa ya kipekee naomba wanawake mliopata fursa hiyo muwe mabalozi kutangaza hizi fursa ya uchimbaji wa madini kwa wanawake, mara nyingi tunaposema fursa za uchimbaji wa madini wanawake wengi utakuta wanajikuta wanapata fursa ya kuwa mama lishe kwenye sehemu za madini, lakini hapa nimefurahi kuna wanawake wadogo wadogo wa uchimbaji wa madini kwa hiyo tuongezeke tuwe wengi,” amesema Nerasi.
Kwa upande wake Afisa Madini Makazi mkoa wa Njombe, Zabibu Napacho akizungumzia lengo la kuwakutanisha wanawake wachimbaji wadogo wa madini mkoani Njombe amesema kuwa wameamua kufanya mafunzo hayo kwasababu wanawake wengi mkoani humo hawajihusisha katika shughuli za uchimbaji wa madini zaidi ya kujikita katika biashara ya chakula na kilimo.
“Wanawake wengi hawana uelewa wa uchimbaji wa madini hivyo wamekuwa na hofu ya kujihusisha na shughuli nzima za uchimbaji wa madini kwa hiyo tulikuwa katika makongamano mbalimbali na walitoa maoni yao kuwa wanahitaji kupata uelewa ili waweze na wenyewe kuingia katika shughuli za madini,” amesema Bi. Zabibu.
Naye mwenyekiti wa chama cha wachimba madini tawi la Njombe, Judith Sanga amesema kuwa mkoa wa Njombe unaongoza sana kwa madini ya viwandani na hivyo wanachokihitaji kwa sasa ni vitendea kazi vya uchimbaji kwa kuwa machimbo mengi ya madini mkoani humo yanahitaji vitendea kazi.
Baadhi ya wanawake wanaopatiwa mafunzo hayo akiwemo Katibu wa Kikundi cha Wanawake Wachimbaji madini Samia (NJOWAMA), Saada Msangi amesema mafunzo hayo kwao yanatija sana kwa kuwa wanawake wa mkoa wa Njombe wameanza kuhamasika kwa kutambua kuwa maisha sasa ni maadili na utajili hivyo hawapaswi kujifunga kuanza kuwa na malalamiko au kutokufanya kazi kwa bidii.