Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu Prof. Peter Msoffe akizungumza leo Novemba 16, 2023 Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda wakati akifungua Kongamano la Kuadhimisha miaka 60 ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) tangu kilipoanzishwa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa akizungumza leo Novemba 16, 2023 katika Kongamano la Kuadhimisha miaka 60 ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) tangu kilipoanzishwa.
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Iren Mtui akizungumza leo Novemba 16, 2023 katika Kongamano la Kuadhimisha miaka 60 ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) tangu kilipoanzishwa.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu imekipongeza Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kuendelea kufanya vizuri katika nyanja mbalimbali na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu kwa ubora wa vyuo vikuu katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akizungumza leo Novemba 16, 2023 Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda wakati akifungua Kongamano la Kuadhimisha miaka 60 ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) tangu kilipoanzishwa, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu Prof. Peter Msoffe, amesema kuwa serikali imejivunia mafanikio makubwa ya MUHAS katika kufanya tafiti za afya na kutoa ushauri wa kitaalam, kuzalisha wataalam wa fani mbalimbali katika sekta ya afya nchini.
Prof. Msoffe amesema kuwa Chuo kikuu MUHAS kinaongoza kwa kufanya tafiti nyingi za afya nchini na kuweza kuleta mapinduzi kwenye sera miongoni inayotumika ndani na nje ya nchi katika kuboresha huduma za afya.
“Tafiti zimechangia katika kukiweka Chuo katika nafasi nzuri kwenye uanishwaji wa vyuo vikuu bora nchini, Afrika na duania” amesema Prof. Msoffe.
Amesema kuwa Wizara inajivunia ukuaji wa Chuo katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu na udahili wa wanafunzi kwani nilianza na wanafunzi 10 kikiwa na programu moja lakini mpaka sasa kina wanafunzi takribani 4,400 na programu za masomo 101.
Prof. Msoffe amesema kuwa mpaka sasa Chuo kimeweza kuzalisha wataalam wa afya zaidi ya 20,000 kwa ngazi ya Shahada za awali ( Stashahada na Shahada) pamoja na zaidi ya wataalam mabingwa 4,200 wa ngazi ya uzamili na uzamivu.
Amefafanua kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa asilimia kubwa na juhudi thabiti, ujasiri, ushirikiano na kujitolea katika kufanikisha maendeleo makubwa katika sekta ya elimu ya afya.
Hata hivyo ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu MUHAS kusimamia kikamilifu mradi wa Elimu ya Juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) ambao utajenga Kampasi ya Mloganzila.
“Uanzishaji wa Ndaki hii unaendana na maono ya chuo ya kufanya mageuzi na kuwa Mji wa Taaluma za afya kufikia mwaka 2050” amesema Prof. Msoffe.
Amesema kuwa ni muhimu kuendelea kutekeleza mradi kwa kuzingatia ratiba na malengo waliojiwekea kulingana na viwango vya serikali na benki ya Dunia.
Ameeleza kuwa mradi wa HEET unakwenda kuongeza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini kwa asilimia 30 katika maeneo 14 ya kipaombele kwa uchumi wetu wa kati na Viwanda.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa wamekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza na kutekeleza tafiti ambazo zimekuwa zikifanyika chuoni hapo.
Prof. Kamuhabwa amesema kuwa matokeo ya tafiti ambazo zimekuwa zikifanyika zimeleta mchango mkubwa katika kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya afya yanayosumbua jamii ya watanzania.
“Katika hatua za kuboresha tafiti, Chuo kumeongeza idadi ya Shahada za uzamili hadi kufikia 84 kwa mwaka 2023 na kuendelea kutoa kipaombele kwa kuwandaa wanafunzi hao ambao ndio msingi wa mkubwa wa tafiti” Prof. Kamuhabwa.
Prof. Kamuhabwa amesema kuwa MUHAS imeendelea kukua na kupanua mazingira ya ufundishaji wa utafiti, huku ikichukua nafasi kubwa katika kutoa ushauri wa kitaaluma kwenye masuala ya afya kwa taasisi mbalimbali.
MUHAS kilianzishwa mwaka 1963 kama Chuo Cha Tiba Cha Dar es Salaam (Dar es Salaam School of Medicine na kipitia mabadiliko mengi na ya Msingi katika kuimarika na ukuaji wake mpaka hadhi ya kuwa Chuo Kikuu kamili kuanzia mwaka 2007.