Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha Mkoani Pwani, imetoa wito kwa wananchi kuacha kujenga kiholela badala yake wafuate utaratibu wa kupata vibali vya ujenzi ili kusaidia kupanga mji .
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji huo, Mshamu Munde akielezea juu ya hoja ya vibali vya ujenzi, wakati wa kikao cha robo ya kwanza kwenye baraza la madiwani Halmashauri ya Mji wa Kibaha ,alieleza wale ambao hawatafuata utaratibu watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria .
Alieleza, kwa kufuata sheria ya kibali cha ujenzi pia itaondoa changamoto ya kubomolewa bomolewa majengo yao.
Munde aliwataka wanaotaka kujenga kwenye maeneo ya Mji huo, waandae michoro ya jengo husika, kutuma maombi kwa mamlaka ya Mji kwa kupata ridhaa ya awali ,kuwasilisha michoro ya jengo na kumbukumbu za kiwanja na kibali kwa maandishi kinachoitwa “Kibali cha Ujenzi”.
Awali Mwanasheria wa Halmashauri hiyo , Charles Lawisso alisema ,kwa mujibu wa kanuni za 124, na 125 za kanuni za Serikali za mitaa ya mwaka 2008 tangazo la Serikali namba 242 la mwaka 2008 ujenzi wowote ndani ya Mamlaka ya upangaji ambazo ni Mamlaka za miji midogo, Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiiji ni lazima upate kibali cha ujenzi kutoka kwenye Mamlaka husika.
Alifafanua, muendelezaji aliyepata kibali anatakiwa kuanza ujenzi ndani ya kipindi cha miezi sita na endapo atashindwa kuanza ujenzi ndani ya kipindi hicho kibali kitakuwa kimeisha muda wake na atatakiwa kuomba kibali upya .
“Kibali cha ujenzi kikishatolewa ujenzi unatakiwa ukamilike ndani ya miaka mitatu (miezi 36) kuanzia tarehe ya kutolewa vinginevyo kinakuwa kimeisha muda wake.”
Lawisso alieleza, endapo ujenzi utakuwa haujakamilika katika kipindi hicho cha miaka mitatu,mwenye kibali anatakiwa aombe kwa halmashauri muda wa nyongeza.
Alitaja adhabu ambazo zinatolewa kwa kujenga bila kibali anakuwa ametenda kosa ,atatiwa hatiani atatozwa faini isiyopungua sh.50,000 na isiyozidi sh.milioni moja au kifungo kisichopungua miezi 12 na isiyopungua miezi 24 au vyote.
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha,Fokas Bundala alieleza katika kipindi cha mwaka 2023/2024 ilikadiria kukusanya Bilioni 48.8 ,Bilioni 7.534 kutoka vyanzo vya ndani.
Alieleza kuwa, katika robo ya kwanza Makusanyo ni asilimia 18 , inaonekana ni kiwango kisichoridhisha na hii imetokana na changamoto ya kutokuwa na elimu ya ulipaji ushuru na baadhi ya vyanzo vya mapato kutokufanya vyema kwenye makusanyo.
Nae Diwani wa Viti Maalum Selina Wilson , alieleza hali ya usafi wa mazingira eneo la Loliondo sio nzuri .
Selina alieleza, Halmashauri iangalie namna ya kuboresha kwenye eneo la usafi na mazingira.
“Halmashauri iangalie namna ya kutafuta fedha hata kwa kukopa ili kumaliza changamoto za Loliondo ,ifanye mchakato kupata fedha ili soko liwe kwenye ubora sanjali na miundombinu yake.”alisisitiza Selina.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Munde alipokea ushauri huo na madiwani kuunga mkono hoja ya kutafuta fedha za kumaliza kero hiyo.
Akitolea ufafanuzi suala la Makusanyo kutofanya vizuri katika kipindi hiki ,alieleza wamejipanga kufanya vizuri kwenye vyanzo vinavyotumia mfumo ambapo Makusanyo ya mwezi Octoba yamefikia zaidi ya milioni 712.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM )Kibaha ,Mwalimu Mwajuma Nyamka aliiomba halmashauri iendelee kusimamia miradi na kuwafikia wananchi.
Nyamka alimpongeza, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mafungu ya fedha “ingekuwa tunategemea vyanzo vya ndani vya halmashauri pekee tungesota ,lakini fedha za Serikali kuu zimekuwa zisaidia kutekeleza miradi ya maendeleo”.
Alieleza, changamoto ya maji bado ni changamoto kubwa ,lakini halmashauri imekuwa haina mkakati wa makusudi, na mjipime ili kumtua ndoo mwanamke,na kutimiza adhma ya Serikali.