Picha no 087 Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 za maji lililojengwa katika mradi wa maji katika kijiji cha Itelefya Halmashauri ya wilaya Momba mkoani Songwe.
Wanyama aina ya Punda wakiwa wamebeba madumu ya maji kutoka kwenye moja ya vituo vya kuchotea maji kilichojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) katika kijiji cha Itelefya wilayani Momba.
Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Itelefya Halmashauri ya wilaya Momba mkoani Songwe wakichota maji katika kituo mojawapo kinachotoa huduma hiyo.
………..
Na Muhidin Amri,
ZAIDI ya wakazi 2,448 wa kijiji cha Itelefya Halmashauri ya wilaya Momba mkoani Songwe,wameondokana na changamoto ya maji baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh.milioni 348.557.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Momba Mhandisi Beatus Katabazi alisema,mradi huo ni miongoni mwa miradi iliyotekelezwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uvico-19.
Alitaja kazi zilizotekelezwa ni ujenzi wa tenki la uwezo wa kuhifadhi lita 100,000,nyumba ya mtambo kwenye kisima(pump house) kuchimba mitaro na kulaza mabomba na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 8 ambavyo wananchi wa Itelefya wanavitumia kupata huduma ya maji safi na salama.
Kwa mujibu wa Katabazi,mradi huo umekamilika na umeanza kutoa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho ambao awali walikuwa katika adha kubwa kwa kwenda hadi mto Momba umbali wa kilomita 1.5 ili kuchota maji kwa ajili ya matumizi yao.
Alisema,mradi huo umetekelezwa kwa njia ya lipa kwa matokeo(P4R) na tangu ulipoanza kutoa huduma umesaidia sana kumtua mama ndoo kichwani na wananchi wa Itelefya sasa wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao na hata kuchochea shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Ruwasa wilaya ya Momba na mkoa wa Songwe kwa ujumla,tunamshukuru sana Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha ambazo zimeleta tija kubwa kwa wananchi wa kijiji hiki na maeneo mengine ya wilaya ya Momba”alisema Katabazi.
Aidha alisema,serikali imetenga kiasi cha Sh.milioni 200 kufanya upanuzi wa mtandao wa maji kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji katika maeneo ambayo hayajapa huduma hiyo wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Katabazi,amewataka wananchi wa kijiji hicho kuvuta maji majumbani badala ya kuendelea kuchota kwenye vituo(DPS),kulipia huduma ya maji ili fedha zinazopatikana ziweze kuboresha huduma na kufanya matengenezo pindi miundombinu ya mradi inapoharibika.
Katika hatua nyingine Katabazi alisema,wamepokea Sh.milioni 500 kutoka wizara ya maji kwa ajili ya kujenga mradi mpya wa maji wa Kamsamba utakaohudumia vijiji viwili vya Kamsamba na Muungano vyenye takribani wakazi 11,250.
Alisema,katika vijiji hivyo kulikuwa na mradi wa zamani uliojengwa tangu mwaka 1978 na ulikuwa unahudumia eneo dogo,lakini kutokana na mahitaji ya sasa mradi ulionekana hauwezi kuhudumia idadi ya watu waliopo kwa sasa.
Alisema,ni matarajio ya Ruwasa kuwa wananchi wa vijiji hivyo wataanza kupata huduma ya maji safi na salama kwenye makazi yao kabla ya mwezi Disemba mwaka huu kwani mchakato wa kuleta mabomba kwa ajili ya kuunganisha maji unaendelea.
Mkazi wa kijiji cha Itelefya Julius Ndege alisema, katika maisha yao hawakuwahi kufikiria kama watapata maji ya bomba kwani tangu kijiji hicho kilipoanzishwa walitumia maji ya mto Momba ambayo hayakuwa safi na salama kwa sababu yalitumika pamoja na wanyama wakiwemo ng’ombe na punda.
Stella Emanuel alisema,mradi huo umesaidia kuimarisha na kuboresha afya zao na kupata muda mwingi wa kushiriki kazi za kujipatia kipato tofauti na hapo awali,ambapo walitumia muda wao mwingi kwenda kutafuta maji.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kamsamba Kyalambwene Kakwale,ameishukuru wizara ya maji ikiongozwa na Waziri Jumaa Aweso kutoa fedha hizo ambazo zinatumika kumaliza changamoto ya maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji vya kata ya Kamsamba.
Kakwale,amempongeza meneja wa Ruwasa wilaya ya Momba Mhandisi Beatus Katabazi kwa kazi nzuri ya kusimamia ujenzi wa mradi huo na kumuomba mkandarasi kuhakikisha anamaliza kazi haraka ili wananchi waanze kupata huduma ya maji kwenye maeneo yao.