Na Sophia Kingimali
Naibu waziri wa fedha Hamadi Chande amesema Tanzania imekuwa kwenye kiwango kizuri cha upatikanaji wa chakula hali iliyopolekea kiwango cha umasikini wa chakula kushuka nchini.
Hayo ameyasema leo Novemba 14,2023 kwenye kongamano la kujadili masuala mbalimbali yaliyojiri wakati wa utekelezaji wa tafiti zilizofadhiliwa chini ya mradi wa benki ya Dunia uitwao living standards measurement study-intergrated survey on Agriculture(LSMS-ISA)ikiwa pia ni maadhimisho ya miaka 15 ya kufanya utafiti ya hali ya umaskini hapa Tanzania na katika Bara la Afrika.
Amesema programu hiyo ya utafiti iliyoanza 2008 ambayo ilifadhiliwa na benki ya Dunia imeleta msaada mkubwa wa kutambua hali ya upatikanaji wa chakula nchini.
“Kiwango cha umasikini kwa sasa kimepungua hasa umasikini wa upatikanaji wa chakula,chakula kipo kwa wingi cha kutosha ambapo sisi watanzania leo tunalisha mpaka nchi jirani”amesema Chande
Kwa upande wake mtakwimu mkuu wa serikali Dkt Albina chuwa amesema miaka 15 ya utafiti huo umeleta mafanikio makubwa ndani ya Bara la Afrika.
Amesema utafiti huo umefanywa kwa kufuatilia kaya moja moja kwa miaka 15.
Amesema kupitia utafiti huo umeiwezesha serikali ya Tanzania na serikali nyingine za Afrika kupunguza umaskini wa chakula.
“Takwimu hizi zimetumika kwenda kwenye program za kuwawezesha watanzania waonyonge hasa maeneo ya vijijini”amesema dk Chuwa.
Amesema wakati utafiti unaanza 2008 katika Bara la Afrika nchi nyingi zilikua zinafanya utafiti kwa kutumia karatasi lakini sasa teknolojia imekuwa na sasa utafiti unafanywa kwa kutukia vishkwambi.
Naye,kamisaa wa Sensa Anna Makinda amewataka watafiti kurudisha tafiti hizo kwa wananchi kwa maana wao ndio wahusika wakuu.
Amesema utafiti huu umefanikiwa kwa sababu umeweza kumfikia mtu mmoja mmoja na kuelezea ukweli kuhusu maisha yake jambo ambalo si rahisi.
“Hawa wataalam wa takwimu tunasema sasa wakati umefika utafiti wao uenze kuwatumikia hawa wananchi lakini pia utasaidia utendaji wa serikali katika kuwahudumia wananchi wake”amesema Makinda.