Mbunge wa Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu tarehe 12/11/2023 ameshiriki mkutano wa hadhara kata ya Mabawa ambao umeandaliwa na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tanga chini ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya Meja Mstaafu Hamisi Mkoba Kabla ya Mkutano huu Mhe Ummy alizindua mashina 6 ya wakereketwa wa CCM katika Kata hiyo.
Katika mkutano huo, Mhe Ummy aliwaeleza wakazi wa Mabawa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambapo alitoa Taarifa ya Miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika kata hiyo kwa kushirikiana na Diwani wa kata ya Mabawa Mhe Mohammed Babu chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Elimu katika Sekondari Mikanjuni na Shule za Msingi za kata ya Mabawa, ikiwemo ujenzi wa madarasa,matundu ya vyoo na maabara,ujenzi wa barabara za kiwango cha lami kutoka Njia panda ya Komesho mpaka Kaskalavila, barabara za changarawe katika mitaa ya Mabawa sambamba.
Pia Mhe Ummy aliwaeleza wakazi wa Mabawa kuwa kwa upande wa huduma za afya wameendelea kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika Kituo cha Afya Mikanjuni na ujenzi wa ukuta katika kituo hicho sambamba na ununuzi wa gari la kubebea wagonjwa kwa fedha zake mwenyewe. Pia Mhe Ummy alieleza jitihada zilizofanyika katika kuimarisha huduma za umeme, maji na masoko katika Jiji la Tanga.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali akiwemo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Ndugu Hamisi Mkoba, Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya, Kaimu Katibu wa CCM Wilaya Ndugu Urasa Nanyaro, Waheshimiwa Madiwani, wajumbe wa kamati ya siasa Kata ya Mabawa wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mabawa Ndugu Hassan Zuberi viongozi na wananchi wa Mabawa na kata za Jirani za Tanga Mjini.