Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. Samia Suruhu Hassan amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila kuwa makundi ya aina yoyote jambo ambalo limeleta tija kwa Taifa katika uongozi wake.
Akizungumza na Wakazi wa Mkoa wa Kagera Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amesema kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakijiita wao ni wa Rais Dkt. Samia jambo ambalo sio kweli kwani yeye hana kundi lolote.
“”Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wanachama wakijirasimisha kuwa wao ni wasamia, Rais Dkt. Samia kundi lake ni Chama Cha Mapinduzi” amesema Makonda.
Makonda amesema kuwa CCM kimekuwa Chama imara kutokana kuwa kimepata kiongozi ambaye ni msikivu, mnyenyekevu na amekuwa akifanya maamuzi kwa kufata kanuni na taratibu za kazi.
“Tunaye Rais Dkt. Samia mpole, mnyenyekevu, asiyekuwa na kundi kutoka sehemu yoyote” amesema Makonda.
Makonda amesema kuwa CCM ni Chama Bora kwa sababu ni Chama chenye utamaduni wa wajikosoa, kujisahiisha pamoja na kubadilika kulingana na mazingira.
Amesema kuwa vipo vyama vingine ambavyo havina uwezo wa kujikosoa hivyo vimekuwa na tabia ya kufukuza wanachama wake.
“Kuna vyama havina uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira, ndiyo maana wapo baadhi ya viongozi walianza wakiwa vijana mpaka sasa ni wazee lakini bado ni viongozi” amesema Makonda.