Siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa kumuhukumu kifungo cha miaka 22 Jela, Maria Ngoda Mkazi wa Mtaa wa Zizi la ng’ombe, Manispaa na Mkoa wa Iringa baada ya kumkuta na hatia ya kukutwa na ndoo yenye vipande 12 vya nyama ya swala kinyume na sheria.
Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) chini ya Mwenyekiti wake Mary Chatanda imesema imesikitishwa na uamuzi huo na itaona jinsi ya kumsaidia Mwanamke huyo kukata rufaa na kumsaidia kupata uwakilishi mzuri ili aweze kupata haki yake.
Tarehe 6 Novemba, 2023 kupitia @AyoTV_ iliripoti kuhusu hukumu hiyo ambayo imetolewa na Hakimu Mkazi Said Mkasiwa baada ya kujiridhisha kuwa ni Kweli Maria alikutwa na ndoo iliyokuwa na nyama hiyo ya swala yenye vipande 12 ndani yake vyenye thamaj ya Tsh. laki tisa ambapo ushahidi uliotolewa umesema siku ya tukio Maria alikutwa na ndoo hiyo yenye vipande 12 vya swala aliyokuwa akiiuza karibu na nyumba yake na hivyo nyama hiyo ikafikishwa kwa Mtambuzi na kubaini ni kweli ilikuwa ni swala na baada ya tathmini gharama yake ikafika Tsh. laki tisa.
Kwa upande wake Mtuhumiwa wakati akijitetea alikiri ni kweli alikutwa na ndoo hiyo ambayo alidai alikabidhiwa na Mtu aliyemtambua kwa jina la Fute na awali hakujua ina nyama ya nini ndani yake “Mheshimiwa ni kweli siku ya tukio nilikuwa kata ya Isakalilo na Mama Ziada nikiuza nyama kwenye ndoo sikujua ni nyama ya nini kulikuwa na vipande 13, kimoja akaondoka nacho yeye” “Baada ya muda Mwenyekiti wa Mtaa akaja na Askari wakaniweka chini ya ulinzi wakisema nauza nyama pori, Mimi nikasema hii ndoo si yangu ni ya Fute wakaniweka kwenye gari hadi kwa huyo Fute, baada yakufikishwa kwa Fute licha ya kumtaja na kumtambua, Uongozi ulinilazimisha nibebe ndoo hiyo na kufikishwa kituoni na kufunguliwa kesi ya kukutwa na nyara za Serikali sambamba na kosa la uhujumu uchumi”
Hata hivyo hukumu hii imeibua hisia mseto kwa Wadau na Wanasheria kutokana na jinsi shauri lilivyoendeshwa kwani Mtuhumiwa hakupata uwakilishi wa kumtetea kipindi chote cha kesi yake hivyo baadhi ya Mawakili wamejitolea kukata rufaa na kumsaidia Mtuhumiwa katika kesi hii.