Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Deogratius Ndejembi amewaelekeza wakuu wa shule za msingi nchini kushirikiana na Wazazi, Walezi na Jamii inayozunguka shule zao ili kulinda usalama wa wanafunzi na kuhakikisha wanadumisha mila,desturi na utamaduni za kitanzania kwa kuwafundisha wanafunzi historia ya Tanzania na kudhibiti matendo maovu yasitokee shuleni.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Novemba 8,2023 wakati wa akifungua mkutano mkuu wa Tano wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania (TAPSHA) na kuongeza kuwa wanapaswa kusimamia nidhamu ya Walimu na Wanafunzi Shuleni wakati wote na kuhakikisha ulinzi wa mali za shule unaimarika wakati wote.
Aidha amewaelekeza Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia na kukamilisha kwa wakati miradi yote kwenye maeneo yao kwa kuzingatia thamani ya fedha na miongozo iliyotolewa.
“Kwa upekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa ajira zikiwemo za walimu ambapo kwa miaka 2 pekee ameajiri jumla ya walimu 22,930 yaani walimu 9,800 kwa mwaka 2022 na walimu 13,130 kwa mwaka 2023. Kati ya walimu hao, Walimu wa Awali na Msingi 12,801 na Walimu 10,129 ni wa Sekondari. Mwenyezi Mungu ambariki sana”amesema Ndejembi.
Sambamba na hayo amaeongeza kuwa Serikali itaendelea kuajiri walimu na watumishi wa kada zingine mbali mbali nchini.
“Ni matumaini yangu kuwa kazi njema inayofanywa na serikali itaendelea kuwa chachu kwenu ya kutimiza majukumu yenu kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ili kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu”, ameongezaa Ndejembi.