Na Sophia Kingimali
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya DCEA imebaini uwepo wa kiwanda cha kutengeneza biskuti zilizochanganywa na bangi katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam pamoja na kukamata kilo 423.54 za bangi iliyosindikwa maarufu kama Skanka.
Akizungumza leo Novemba 8, 2023 jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema kufuatia operesheni maalum zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi ndio imefanikisha kukamata Skanka hiyo.
Hivyo Lyimo amesema wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wanapaswa kuwa makini na vyakula hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto
Amesema kilo 158.54 zilikamatwa eneo la Kigamboni na Kawe jijini Dar es Salaam zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mabegi ya nguo tayari kwa kusafirishwa huku kilo 265 zilikamatwa katika matukio tofauti mikoa ya nyanda za juu Kusini zikiwa zimefichwa ndani ya magari kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine ikiwemo maboksi yenye matunda aina ya Apples zikisafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam.
Aidha Mamlaka hiyo imewataka watu wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti kwa kuchanganya na Skanka katika eneo la Kawe huku akifafanua katika tukio hilo watuhumiwa walikutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga skanka na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi kusitisha uzalishaji huo.
“Kutokana na operesheni hizo watu 16 wamekamatwa ambapo kati yao sita wamefikishwa mahakamani na 10 watafikishwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika lakini pia Mamlaka imebaini maeneo yanayotumika kama masoko ya kusambazia na kuuza Skanka kwenye fukwe ya Bahari ha Hindi”
Akifafanua kuhusu Skanka( Skunk) amesema ni jina la mtaani linaloitambulisha aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu ikilinganishwa na bangi ya kawaida.
Ameongeza dawa hiyo ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto ambapo asilimia 75 ni bangi aina ya Sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya Indica.”Kiwango cha sumu kilichopo kwenye sanka ni zaidi ya asilimia 45 ukilinganisha na bangi ya kawaida ambayo kiwango chake cha sumu ni kati ya asilimia 3 mpaka 10.
Ameongeza kuwa Skanka ina madhara makubwa zaidi kwa mtumiaji ikiwemo kuamsha na kuzidisha magonjwa ya afya ya akili kwa haraka.Imebainika kuwa watu wasiowaaminifu huchanganya sanka kwenye vyakula kama vile biskuti, keki, jamu , sharubati , tomato souce pia kwenye sigara na shisha.
” Lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha uuzwaji wa dawa hizo kwa kuficha na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto, “amesema.
Pamoja na hayo amesema Mamlaka hiyo inaendelea kufanya operesheni dhidi ya wasafirishaji na wazalishaji wa dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha dawa za kulevya haziendelei kuwepo nchini.
” Tunawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga namba ya bure ya 119 ambapo taarifa zitapokelewa kwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi.”amesema
Aidha amesema kutokana na kufanyika kwa operesheni ya kutokomeza dawa za kulevya nchini hivi sasa wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa hizo kuingiza bangi kutoka nchi nyingine lakini Mamlaka imeimarisha ulinzi mipakani ili kuhakikisha hakuna dawa za kulevya zinazoingia nchini.