WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka viongozi wa Chama Cha Gofu Tanzania (TGU) na Chama cha Gofu Wanawake Tanzania (TLGU) waandae Mkakati wa kuziwezesha timu za Taifa za vijana chini ya umri wa miaka 14 na 20 (U14 na U20) na timu za wakubwa za wanaume na Wanawake kushiriki na kushinda mashindano ya Kimataifa .
Waziri Dkt. Damas Ndumbaro ametoa Rai hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa kwa timu ya Taifa ya Gofu Wanawake lililopatikana baada ya timu hiyo kufanya vizuri na kutetea ubingwa wao katika Mashindano ya Gofu Afrika Mashariki na Kati yaliyomalizika Novemba 3, 2023 Kigali nchini Rwanda.
Amesema lengo la kuandaliwa kwa mkakati huo ni kuwezesha kubaini vipaji na kuhakikisha kuwa timu za Taifa za Tanzania za mchezo wa Gofu zinakuwa na maandalizi mazuri na kuwa na wawakilishi watakaopata nafasi ya kushiriki katika Mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi na kuliletea heshima Taifa.
” Natoa agizo kwa Vyama vya Mchezo Gofu Wanaume na Wanawake vijipange, tunahitaji timu ambazo wachezaji wake watapata nafasi ya kucheza kwenye timu ya umri wa miaka 20 (U20) pia kucheza kwenye timu za wakubwa ambao watachukua nafasi ya hawa waliopo sasa kwa miaka ya baadaye,” amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Waziri Ndumbaro amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) italeta wataalam wa nje kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wachezaji ili kuwanoa na kuwaongezea ujuzi akiongeza kuwa wachezaji wenye vipaji wanahitaji kuweka kambi katika nchi zinazofanya vizuri pia kuzoea hali ya hewa ya nchi tofauti.
Aidha, amesisitiza kuwa wachezaji hao wa Timu za Taifa za Tanzania wanahitaji kuendelea kupatiwa mafunzo na ujuzi ili wafikie viwango vya juu zaidi Duniani kwa kuwa ndani ya Bara la Afrika hawana mpinzani.
” Kwa Sasa Serikali tumeweka utaratibu tunapoikabidhi timu Bendera ya Taifa kwenda kushiriki Mashindano nje ya nchi pindi inaporejea ieleze kwa umma wa Watanzania imefanya nini katika ushiriki wake ,hivyo timu zote mjipange msiwe watalii bali mkapambane,” amesisitiza .
Naye Rais wa TLGU Queen Siraki amesema mazoezi, nidhamu, uzoefu na uzalendo ndio siri kubwa ya kutwaa ubingwa huo akibainisha kwamba timu hiyo ipo vizuri na wanaendelea kuangalia namna ya kupata timu B ambayo itakuwa mbadala na mpango huo utawasilishwa BMT.
Naye Nahodha wa timu ya Gofu ya Wanawake Hawa Wanyeche amesema kuwa mashindano yaliyomalizika yalikuwa na mazuri na yalikuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa kila timu ilijipanga kutetea nchi yake na kurudi na ushindi.
” Tunaishukuru Serikali kwa kutuwezesha kushiriki katika Mashindano hayo licha ya kuwepo kwa changamoto ya mvua nyingi wakati wa mchezo timu yetu ilijipanga vizuri kuitetea nchi na sisi tuliweza kuchukua ubingwa ,” amesema Hawa.