Na Sophia Kingimali
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kinondoni imewataka wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo kuwasilisha kwa Mamlaka ya Mapato TRA shilingi millioni 89,426,979.39 Kwa Halmashauri ya kinondoni na shilingi 53,832,188.16 kwa Halmashauri ya ubungo ambazo zilikatwa kwa ajili ya kodi ya zuio kwa bidhaa za huduma kwa mwaka 2021/22 na 2022/23.
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam novemba 7,2023 na Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Elizabeth Mokiwa wakati akiwasilisha taarifa na ya Utendaji kazi Kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Septemba 2023 kwa waandishi wa habari.
“Uchambuzi wa mfumo kuhusu ukataji na uwasilishaji wa Kodi ya zuio katika ununuzi wa vifaa na huduma katika Halmashauri za Manispaa Kinondoni na Ubungo ulilenga kuboresha na kuimarisha matumizi ya risiti za EFD na ukataji wa kodi ya zuio kwenye manunuzi ya huduma na vifaa katika Halmashauri “amesema.
Naibu Mkuu huyo wa Takukuru mkoa wa Kinondoni aliendelea kueleza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu imefanikiwa kufatilia miradi 11 yenye thamani ya shilingi 3,732,846,664.00.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa programu ya Takukuru rafiki amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa kuzifikia kata 6 ambapo katika vikao na wadau kero 29 zikiweza kuibuliwa na kati yake tayari kero 10 zimepatiwa ufumbuzi.
Pia ameongeza kuwa katika kipindi hicho Takukuru mkoa kinondoni imepokea jumla ya malalamiko104 ambayo yalihusu Rushwa ni 59 na yasiyohusu Rushwa 45.
“Katika kipindi husika mashauri mapya mawili yamefuguliwa mahakamani huku mashauri matatu yalitolewa maamuzi na Jamhuri ilishinda katika shauri moja hivyo kufanya jumla ya kesi zinazoendelea mahakamani kuwa 21″amesema Mokiwa
Katika hatua nyingine Naibu Mkuu huyo amesema Takukuru Mkoa wa Kinondoni imekuwa ikihakikisha inatoa huduma inayowafikia wananchi wote .
“Tunaendelea utekelezaji wa programu ya Takukuru rafiki kwa kuendeleza ushirikiano na wananchi pamoja na wadau wote wanaohusika na kutoa na kupokea huduma .
Ameongeza kuwa Takukuru mkoa wa Kinondoni ilishiriki katika Uzinduzi wa Kampeni ya vunja ukimya kataa Rushwa ya ngono Kwa waandishi wa habari wa kike ambayo iliandaliwa na Taasisi ya Tanzania media women Association TAMWA .
Amesema kampeni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani imesaidia kudhibiti rushwa ya ngono kwa waandishi wa habari.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Takukuru kuibua vitendo vya Rushwa katika maeneo yao kupitia programu ya Takukuru rafiki ili kuzuia na kumaliza kabisa swala la rushwa nchini.