Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (mbele katikati) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour (wa pili kulia) na Viongozi wengine wa Wizara na Taasisi zillizo chini ya Wizara hiyo akikata utepe kufungua Jengo la Ofisi za Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Mhandisi Annex) jijini Dodoma, tarehe 07 Novemba 2023.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (wa pili kulia) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour (kulia) na Viongozi Viongozi wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) akiweka jiwe la Ufunguzi wa Jengo la Mhandisi Annex, jijini Dodoma, tarehe 07 Novemba 2023.
Mwonekano wa Jengo la Mhandisi Annex ambalo ni Ofisi za Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) lililofunguliwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, jijini Dodoma tarehe 07 Novemba 2023.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na Viongozi na washiriki wa hafla ya ufunguzi wa jengo la Mhandisi Annex ambalo ni Ofisi za Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), jijini Dodoma tarehe 07 Novemba 2023.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (mbele katikati) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour (wa pili kushoto) na Viongozi wengine wa Wizara na Taasisi zillizo chini ya Wizara hiyo akiwa katika picha ya pamoja na Bodi ya Usajili wa Wahandisi mara baada ya kufungua Jengo la Mhandisi Annex, jijini Dodoma, tarehe 07 Novemba 2023.
……………………………
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuiwezesha na kuiendeleza taaluma ya kihandisi ili kuongeza ushindani katika Soko la ndani na nje ya nchi.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma mara baada ya kuzindua jengo jipya la Bodi hiyo “Mhandisi Annex” ambalo limejengwa na wahandisi wazawa.
Bashungwa amesema kuwa Serikali bado ina uhitaji mkubwa wa wahandisi kwani Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anahakikisha anaifungua nchi kutokana na uwekezaji mbalimbali anaofanya kupitia miradi mbalimbali, kwa namna moja ama nyingine wahandisi wanahitajika kwa wingi ili kutekeleza miradi hiyo.
“ERB muendelee kusimamia taaluma hii, Watanzania tunaitegemea katika kuendeleza nchi yetu, tuijenge nchi yetu katika namna ambayo mchango wa Mhandisi utaonekana katika kuifanya Tanzania ipendeze na kuwa sehemu ya kuigwa”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaandaa mpango mkakati wa kuwajengea uwezo wataalamu wake ili waweze kutekeleza miradi hiyo na kuweza kuleta tija kwao na Taifa kwa ujumla.
Aidha, ameiagiza Bodi hiyo kuendelea kuiheshimu na kuitendea haki taaluma hiyo kwa kuhakikisha miradi wanayoitekeleza inakuwa bora na yenye viwango.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Eng. Menye Manga, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya Waziri huyo ambapo amesema kuwa watahakikisha wanafuata, sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao.