Na.Jacob Kasiri – Iringa.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi – TANAPA, Godwell Meing’ataki Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha, amekabidhi magodoro 41 yatakayotumika kwa ajili ya malazi kwa wafungwa wanaotumikia makosa mbalimbali katika Gereza Kuu la Iringa lililoko mjini Iringa.
Magodoro hayo 41 yatakuwa na mchango mkubwa na kutoa ahueni ya malazi kwa wafungwa wanaotumikia makosa mbalimbali katika gereza hilo.
Akikabidhi magodoro hayo, Kamishna Meing’ataki alisema, “Msaada huu ni mchango wa faida zinazotokana na utalii. Mara nyingi tumekuwa tukijihusisha zaidi na miradi ya maendeleo kwa wananchi wanaozunguka hifadhi zetu, hivyo kwa leo tumeona tutoe magodoro ikiwa ni mchango wetu kwa wenzetu wanaotumikia makosa yao.”
Aidha, Kamishna huyo aliongeza kuwa msaada huu ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na Gereza Kuu la Iringa na pia, kama TANAPA tunawathamini sana ndugu zetu walioko magerezani.
Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Daniel Mwakapila, Mkuu wa Gereza la Iringa alisema, “TANAPA ni wadau wazuri sana kwetu na tunashirikiana nao katika mambo mengi, pia tuwashukuru kwa msaada huu ambao utatuondolea adha iliyokuwepo licha ya kwamba hautamaliza tatizo lote ila utasaidia kwa kiasi kikubwa”.
Magodoro hayo 41 yamekabidhiwa leo tarehe 06.11.2023 katika Gereza Kuu la Iringa.