…………………….
Na Sixmund Begashe
Wananchi wametakiwa kuwapa ushirikiano Askari wa Wanyamapori Vijijini (VGS) ili waweze kutekeleza Majukumu yao vizuri ya ulinzi wa Maliasili pamoja na kuwalinda wanavijiji dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba kwenye ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii nyanda za juu Kusini (REGROW) kupitia vikundi vya Kijamii vya COCOBA na Miradi ya kuzalisha kipato katika Kijiji cha Chinungulu Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Kamishna Wakulyamba amesema kuwa uwepo wa askari wa VGS ni mpango mzuri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mradi wa REGROW wa kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na Uhifadhi endelevu wa Maliasili nchini hivyo dhamira hiyo inapaswa kuungwa Mkono kwa wananchi kushirikiana vyema na askari hao.
Akizungumzia mchango wa REGROW katika Kijiji cha Chinugulu, Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw. Daniel Njelula, amesema, askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) wamekuwa msaada mkubwa katika kueleimisha jamii juu ya kuwadhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu, na pia kuwafanya wananchi kuachana na ujangili hivyo ameushukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wa Kijiji hicho kupitia mradi huo.
Naye Katibu Msaidizi wa kikundi cha AMANI, Bi Upendo Vuliva amesema miradi ya REGROW imeimararisha upendo na furahaa kwenye familia kwa kuwa inawawezesha wanawake kuchangia katika pato la familia tofauti na awali familia nyingi wanaume pekee ndio walikuwa watafutaji kwaajili ya familia zao.
Naye Msimamizi wa Kipengele cha pili cha Mradi wa REGROW Bi. Hobokela Mwamjengwa ameeleza kupitia mradi huo, Shilingi 435,382,570 zimetumika katika vijiji 3 vinavyopakana na hifadhi ya Taifa Ruaha kwa upande wa Mkoa wa Dodoma, kwa kutoa fedha mbegu kwenye vikundi 10, miradi ya kuzalisha kipato 10, kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 18 na mafunzo ya Askari Wanyamapori wa vijiji 29