Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa wito kwa wafanyabiasha na Makampuni yenye uwezo wa kusafirisha Korosho nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara kujitokeza kuomba leseni za usafirishaji kutokana na Serikali kufanya maboresho makubwa katika Bandari hiyo kwa sasa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge tarehe 04 Novemba, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu taarifa kuwa Wizara ya Uchukuzi kupitia Shirika hilo linazuia kutoa Leseni kwa wafanyabiashara wanaotaka kusafirisha Korosho nje ya nchi.
Bw. Mkeyenge ameongeza kuwa, tangu wameanza kutoa leseni hadi kufikia Novemba 03, 2023 Makampuni 207 yamepewa Leseni ambapo tani zaidi ya 5,300 zinatarajiwa kusafirishwa nje ya nchi.
“Kumekuwa na ujumbe ukitembea kuhusu Wizara na taasisi yake kwamba tumekuwa tukifanya ugumu katika kutoa leseni kwa wafanyabiasha ili kuweza kusafirisha korosho, niseme tu hili sio kweli kwani hadi sasa TASAC tayari tumeshatoa leseni kwa Kampuni takribani 207, na tani zaidi ya 5000 zinatarajiwa kusafirishwa. ” Amesema Mkeyenge.
Amesisitiza kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha sekta ya Kilimo inakua sambamba na kuimarisha mazingira ya Biashara ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema kuwa TASAC itaendelea kutekeleza maagizo ya Serikali pamoja na kusaidia wananchi kufikia malengo, kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.