Joseph K. Edward – Ngorongoro
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe.Raymond Mwangwala, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari Masusu, kata ya Pinyinyi na kuridhishwa na hatua za utekelezaji wa mradi huo na kuwapongeza mafundi na wananchi wa Pinyinyi kwa kujitoa kutekeleza mradi huo, huku akiagiza kukamilika kwa jengo la utawala ndani ya siku tatu.
Aidha ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za kutekeleza na kukamilisha miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo, huku mradi wa shule ya Masusu sekondari ukiwa ni neema na nuru kwa watoto wa Panyinyi.
“Mhe. Rais ameendelea kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo kisekta miradi ambayo inalenga kutatua changamoto nyingi za wananchi wa Ngorongoro, hivyo ni jukumu letu kusimamia miradi na kuhakikisha miradi yote inaleta matokeo yaliyokusudiwa na Serikali” Amesema Mhe. Mangwala.
Naye mwenyekiti wa kitongoji cha Masusu, Mhe. Daniel Taiko Mollel ameishukuru Serikali ya awamu ya sita, kwa ujenzi wa shule mpya ndani ya kitongoji chake, shule ambayo licha ya watoto kusoma karibu na nyumbani itaondoa changamoto ya watoto kuacha shule hususani watoto wa kike wanaokabiliwa na changamoto ya ndoa za utotoni.
“Sisi wananchi wa Masusu, tunajisikia furaha kwa kujengewa shule ya sekondari, hatukuwahi kuwa na shule kijijini kwetu, tunajivunia kuwa na Rais mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatujali kama watoto, tunamshukuru sana kwa kutukumbuka” Amebainisha
Kiongozi wa mila, Laigwan Joshua Mang’atinda, hakusita kutoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya sita kwa kujenga shule ya sekondari Masusu na kumshukuru mkuu wa Wilaya na watalamu wake kwa usimamizi wa karibu na kuhakikisha mradi unakamilika kwa kuzingatia vigezo vya ubora.
” Watoto wetu walilazimika kutembea umbali wa Km 10 mpaka 15 kufuata shule kata za jirani, mradi huu ni mkombozi wa watoto wetu, tuko tayari kufanya kazi usiku na mchana ili shule hii ikamilike haraka na watoto wetu waanze kusoma mapema ifikapo Januari 2024″ amehitimisha Lagwanan.
Sevelin Erasto mwalimu wa shule ya sekondari Sale na msimamizi wa mradi huo, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia mradi wa Kuboresha miundombinu ya shule za Sekondari Nchini (SEQUIP) kwa gharama ya shilingi milioni 584.2
Ikumbukwe kuwa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020. Ibara ya 77,
“CCM inaamini kuwa elimu bora ndiyo nyenzo muhimu ya kujenga, kulea, na kuendeleza rasilimaliwatu ili kuchangia kikamilifu ujenzi wa Taifa na maendeleo ya jamiikwa ujumla”.