Siku ya mwisho ya ziara ya Mfalme Charles III nchini Kenya ilitatizwa siku ya Ijumaa na mvua kubwa na mafuriko alipotembelea kitovu cha kihistoria cha mji wa pwani ulio katika Bahari ya Hindi wa Mombasa.
Hali mbaya ya hewa ilivuruga mipango ya safari ya Charles na Malkia Camilla na kuwafanya wapande bajaji ya umeme maarufu kama ‘Tuktuk’ kwenda Fort Jesus, eneo la Turathi ya Dunia la UNESCO la miaka 400 katika Mji Mkongwe wa Mombasa.
Badala yake, wanandoa hao wa kifalme walisimama kwa muda mfupi na kupiga picha ndani ya gari la magurudumu matatu, ambalo lilikuwa limepambwa kwa muundo wa Kiafrika na nembo ya Union Jack.
Pwani ya Kenya na maeneo mengine ya nchi yamekuwa yakikumbwa na mvua kubwa na wakati mwingine katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mafuriko.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP