Na. Edmund Salaho- Kilimanjaro
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbas amebanisha kuwa mwanzoni mwa mwezi Disemba, 2023 magwiji wa mchezo wa tennis duniani watakuja kuoneshana umwamba katika mchezo huo unaotarajiwa kufanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitia programu maalumu ilioanzishwa na kampuni ya utalii ya Gosheni Safari ijulikanayo kama ‘Epic Tanzania Tour’.
Dkt. Abbas ameyasema hayo wakati akizungumza na wanahabari baada ya mapokezi ya wawekezaji zaidi ya 150 kutoka Taifa la Marekani walioingia nchini leo kwa ajili
ya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta ya utalii.
“Leo tumewapokea wawekezaji zaidi ya 150 kupitia programu iliyoanzishwa na kampuni ya Gosheni Safari inayojulikana kama ‘Epic Tanzania Tour’ ambapo tumeshuhudia wawekezaji mbalimbali wakiingia nchini kutokea jana lakini wageni wanaokuja Disemba Serengeti dunia itasimama, hawa ni magwiji wa mchezo wa Tennis duniani na wanatarajia kutumia siku 10 ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti” alisema Dkt. Abbas.
Miongoni mwa watopezi wa mchezo wa Tennis wanaotarajiwa kuwasili nchini ni Gigi Fernandez, John McEnroe pamoja na Mac Roy ambao wanatarajiwa kushiriki mchezo huo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti mwanzoni mwa Disemba.
Aidha, Dkt. Abbas amewapongeza Gosheni Safari na kutoa wito kwa sekta binafsi kuiga mfano wa Kampuni hiyo katika kumuunga mkono rais wetu kupitia filamu ya The Royal Tour na kubainisha kuwa kuzaliwa kwa ‘Epic Tanzania Tour’ ni mfano hai wa uwekezaji uliofanywa na Rais Samia kupitia Filamu ya Royal Tour.
“Tunapoona wageni hawa nchini ni uwekezaji uliofanywa na Rais kupitia filamu ya Royal Tour tuendelee kumpongeza na kumtia moyo Rais wetu aendelee kufanya mengine makubwa kwani kwa sasa tumevunja rekodi ya kwanza kwa kufikisha watalii wa nje million 1.6 na rekodi ya pili tumeivunja kwa kufikisha mapato kiasi cha dolla billioni 3.07 ambayo ni zaidi ya Trillioni 7”.
Kwa upande wake Bw.Peter Robert, ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Gosheni Safari alibainisha kuwa ujio wa wawekezaji wa hawa pamoja na wacheza Tennis mwezi Disemba umetokana na juhudi za Mhe. Rais Samia kupitia filamu ya Royal tour.
“Wawekezaji hawa walitamani kufika Tanzania kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji baada ya kuona filamu ya Royal Tour ambayo aliifanya Rais sisi kama Gosheni Safari tulikutana nao wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo nchini Marekani”. Alisema Bw. Peter.