Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga Novemba 3, 2023 alitembelea na kutoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya awali na Msingi inayofahamika kwa jina HolyLand Pre & Primary School iliyopo Mji mdogo wa Makongolosi Wilayani Chunya.
Akizungumza na walimu na wanafunzi Shule hiyo, Kamanda Kuzaga amesisitiza na kuwataka wanafunzi kuzingatia yale yote wanayofundishwa pamoja na kutojihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi, ulawiti pamoja na vitendo vyote vinavyopelekea mmomonyoko wa maadili.
Aidha, Mkuu wa dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Mbeya Mkaguzi wa Polisi Lovenes Mtemi amewataka wanafunzi kutokaa kimya na kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi yao na kuwataka kutoa taarifa mapema kwa walimu, wazazi na Jeshi la Polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.
Naye, Kaimu Afisa Elimu mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongolosi ndugu Donald Mwambeule amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya na kuomba elimu waliyoitoa iendelee kutolewa kwa wanafunzi wa Shule nyingine ili kuwajengea uelewa na kujiepusha na vitendo vya uhalifu.
Aliongeza kuwa, anapongeza jitihada za uongozi wa Shule hiyo kuajiri walimu/wataalam wa masuala ya saikolojia ili kuwasaidia watoto na kuwajenga vizuri katika masomo yao na hata kubaini changamoto walizo nazo na kuzitafutia ufumbuzi.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Shule hiyo ndugu Lawena Nsonda @ Baba Mzazi amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kufika na kutoa elimu kwa wanafunzi kwani elimu hiyo itasaidia sana kupunguza vitendo vya uhalifu hususani ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto na kupelekea watoto kufunguka kutoa taarifa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa elimu mbalimbali kwa wanafunzi na Jamii kwa ujumla kupitia vituo vya redio, mashuleni pamoja na mikutano ya hadhara ili kuzuia matukio ya uhalifu ndani ya Mkoa wa Mbeya.