Wataalam kutoka Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO ) wamekutana na kufanya mazungumzo na wataalam wa kiwanda cha uzalishaji wa Unga cha Bakhresa kilichopo eneo la TAZARA jijini Dar Es Salaam.
Ziara hiyo inafuatia juhudi mbali mbali zinazofanywa na TIRDO kwa ajili ya kuwafikia wadau wa Viwanda nchini lengo ni kuona namna ya sekta viwanda nchini inavyofanya kazi lakini pia kuwakaribisha wadau wa Sekta ya Viwanda kutumia tafiti mbali mbali zinazofanywa na wataalam wa TIRDO.
Kiongozi wa Msafara huo Bwana Ndos Humphrey Ndosi ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO Prof. Mkumbukwa Mtambo alitumia fursa hiyo kufafanua majukumu Mahsusi ya TIRDO na namna ambavyo wanaweza kuwasaidia kufikia maendeleo makubwa kutokana na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia yanayoendelea kote duniani.
Bwana Ndosi aliwakaribisha wataalam hao wa Bakhresa kufika TIRDO kupata huduma ikiwa ni pamoja na kutumia maabara za kisasa zilizopo katika Shirika hilo kama vile Maabara ya chakula , maabara ya Kemia pamoja na maabara ya nishati.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Kiwanda cha unga cha Bakhresa Bwana Iddy Mvungi alisema kuwa wamefurahia ziara hiyo na kuahidi kuanza ushirikiano na Shirika hilo.
Bwana Mvungi alitaja maeneo matatu ya kuanza ushirikiano kuwa ni Nishati , Mfumo wa mawasiliano pamoja na Maabara. “Nimefurahi sana kusikia kuwa mna maabara bora ya vyakula , sisi ni wazalishaji wakubwa wa biadhaa za chakula, tupo tayari kutumia maabara zenu na wataalam kutoka TIRDO ili tuweze kufikia masoko makubwa ya ndani na nje ya nchi kwa ubora wa hali ya juu’’ aliongeza Bwana Mvungi.
Mtaalam mwingine kutoka Bakhresa Bwana Sudhakar Akella alisema kuwa wao kama wazalishaji ambao ni watumiaji wakubwa wa Umeme nchini wamefurahi kusikia kuwa TIRDO wanao wataalam wanaoweza kuwasaidia kupungunguza gharama za matumizi na pia kufikia matumizi bora ya umeme.
“Viwanda vinatumia umeme mwingi na ni gharama kubwa , pamoja na kuwa tunao wataalam lakini tupo tayari kushirikiana nanyi kwa ajili ya wataalam wenu kutusaidia’’ aliongeza Bwana Sudhakar.
TIRDO kama Shirika la utafiti na Maendeleo ya Viwanda imejikita katika kufanya tafiti mbali mbali za kibingwa kwa kuwatumia wataalama wake wabobevu waliopata mafunzo ndani na nje ya nchi kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi.
Timu ya Wataalam kutoka TIRDO iliongozwa na Bwana Humphrey Ndosi (Kaimu Mkurugenzi wa utafiti wa Viwanda), Dr. Masoud Masoud (Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA) ,Dr. Purificator Kiwango (Mtafiti na mtaalam wa Maabara ya vyakula), David Langa (Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Shirika na Mipango) , Eng.Augustine Masse (Mtafiti na mtaalam wa Nishati), Bi Elizabeth Mtegwa (Mtafiti na mtaalam wa TEHAMA )pamoja na Bw. Burhan Mdoe (Afisa Masoko).