Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Nov 3
MKURUGENZI wa idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi ,ameielekeza mikoa na halmashauri hizo, kueleza makubwa yanayofanywa na Serikali ili kuondoa maswali kutoka kwa wananchi juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoelekezwa kwenye maeneo yao.
Aidha ameitaka mikoa na halmashauri hizo kusimamia kikamilifu mabilioni ya fedha yanayopelekwa na Serikali, kutekeleza miradi ya maendeleo ili iweze kuleta tija.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari pamoja na viongozi wa mkoa wa Pwani ,Matinyi alieleza, bado kuna pengo kwa wananchi, kati ya wanachokiona na kinachofanywa na Serikali yao.
Kadhalika Matinyi ,ameutaka mkoa wa Pwani kuongeza kasi ya kutangaza fursa za uchumi wa bluu ,ambao utafungua uchumi wa Mkoa.
“Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo, kujenga miradi mingi kila kona ya nchi ,lakini wananchi hawaelezwi michanganuo na utekelezaji wa ilani unavyotekelezwa “alifafanua Matinyi.”
Akitolea ufafanuzi juu ya mikutano ya aina hii ambayo imezinduliwa Dodoma,na kufanyika Morogoro na Pwani hadi sasa ,Matinyi alieleza ni mpango endelevu mikoa yote , kueleza utekelezaji wa miradi ya Serikali katika kipindi cha kuanzia 2021-2023.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alieleza, katika kipindi cha miaka mitatu mkoa huo, umepokea sh. Trilion 1.19 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Fedha hizi zimetumika kutekeleza miradi ya afya, Elimu, Maji na miundombinu na hivyo kupunguza kero kwa wananchi”
“Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa, kuufungua mkoa, dhamira yake mkoa kuwa wa kimkakati,Sisi hatutomuangusha ,kwani tumejipanga kwakuwa tuna fursa za kutosha”alieleza Kunenge.
Kuhusu miundombinu ya barabara Kunenge alieleza, Serikali ipo mbioni kuanza ujenzi wa upanuzi wa barabara kuanzia Dar es Salaam-Chalinze-Morogoro.
“Barabara hii inakwenda kupunguza changamoto ya msongamano wa magari ,ajali ambao huwa ukijitokeza “
Kunenge alifafanua pia ujenzi wa barabara ya Chalinze-Utete ambayo itafungua milango ya kiuchumi na maendeleo katika maeneo hayo.
Upande wa uwekezaji na viwanda , alieleza, Mkoa una viwanda 1,525 ambapo viwanda vikubwa 120,vya Kati 120 huku viwanda 30 vikiwa vimeanzishwa ,kongani 23 na mji wa kibiashara na uwekezaji Kwala.
“Hii ni fursa kubwa kwakuwa tutainua sekta ya uwekezaji,mkoa na Taifa kujiongezea pato la Taifa na kuongeza ajira”alisisitiza Kunenge.
Katika afya Kunenge alisema kuwa ,kati ya fedha hizo bilioni 30.58 zimeenda kutekeleza miradi ya afya , upatikanaji wa dawa kwa sasa ni asilimia 93.
Elimu imepokea Bilioni 63.5 kuboresha sekta hiyo ,:;”sekta ya maji Bilioni 423.8 hivyo upatikanaji wa maji asilimia 86.
Kunenge anasema, Nishati ya Umeme amesema kituo cha kupoozea umeme Chalinze kimefikia asilimia 85 na ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere umekamilika kwa asilimia 93.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti Hemed Magaro alieleza, wamepokea katika kipindi hicho Bilioni 20.34 kati ya fedha hizo bilioni 5.9 zimeenda katika sekta ya afya ambapo milioni 750 zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
“Vituo vya kutolea huduma vimeongezeka kutoka 63-74 ,ambapo katika upande wa eneo la Mbwera kulikuwa hakuna kituo cha afya wakazi walikuwa wakitembea km 90 kufuata huduma za kiafya hatua ambayo imepunguza vifo vya uzazi kwa mama na mtoto kutoka 51 hadi 31″alieleza Magaro.
Katika hatua nyingine, Meneja wa wakala wa barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mkoa wa Pwani, Leopold Runji alieleza, mkoa umepokea Bilioni 84 .
Alieleza, hadi sasa mtandao wa
barabara kwa kiwango cha lami km 95.6 kati ya hizo ni ongezeko la km 40 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Runji alieleza,wanaboresha mtandao wa barabara kwani hadi sasa kiwango cha changarawe km 556- kufikia 1,600.