Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameungana na Rais Haikande Hichilema wa Zambia kukutana na Viongozi mbalimbali wa Ufalme wa Lesotho kama sehemu ya mchakato wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa na kiusalama uliopo katika Ufalme wa Lesotho.
Viongozi hao wawili wapo nchini Lesotho kutekeleza maagizo ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ya kuusaidia Ufalme huo kukamilisha mchakato wa kutafuta amani ya kudumu katika Ufalme huo ambao haujawahi kupata amani ya kudumu tangu ulipopata uhuru hadi sasa.
Rais Hichilema ameongoza ujumbe huo kama Mwenyekiti wa sasa wa Ogani ya Utatu ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Umoja wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ Troika). Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameambatana naye kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Jopo la Wazee la SADC (POE) ambapo ndiye aliyekabidhiwa jukumu la kuongoza timu ya usuluhishi wa mgogoro huo wa Lesotho.
Pamoja na mambo mengine, Viongozi hao wamepata fursa ya kuonana na Mfalme Letsie III wa Lesotho, Waziri Mkuu wa Nchi hiyo Mhe. Samuel Makane pamoja na Viongozi wa Vyama vya Upinzani nchini humo.
Katika Mkutano wao na Waziri Mkuu Sam Matekane Viongozi hao walipokea taarifa ya Serikali ya Ufalme huo katika kutekeleza mchakato wa kupitisha Bungeni muswada wa mabadiliko ya kudumu unaoaminika na wengi kuwa ndiyo muarobaini wa kudumu wa changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hiyo. Waziri Mkuu huyo alielezea nia ya dhati ya Serikali yake kusimamia na kuhakikisha kuwa muswada huo unapitishwa kama inavyotarajiwa na wengi.
Aidha, katika kikao na Viongozi wa Umoja wa Upinzani Viongozi hao walipata fursa ya kusikiliza masuala ambayo upande wa Upinzani wanaamini ni vyema yakafanyiwa kazi ili mchakato huo uweze kukamilika kwa kuzingatia maoni ya wadau wote.
Kwa upande wao, Rais Hichilema na Rais Mstaafu Kikwete walitumia fursa ya kukutana na Viongozi hao kusisitiza umuhimu wa pande zote zinazohusika katika kutafuta suluhu ya kudumu nchini humo kutanguliza maslahi mapana ya Ufalme wa Lesotho ili kukamilisha mchakato huo uliofikia katika hatua nzuri ya majadiliano. Aidha, walisisitiza haja ya pande zote husika kuwa na mtizamo wa kufanya maridhiano ya kisiasa hususan katika masuala magumu wanayoshindwa kufikia muafaka ili kuepusha kuurefusha mchakato huo bila sababu za msingi.