Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutoa elimu mara kwa mara juu ya mwenendo wa ukarabati wa mitambo yao ili kuepusha malalamiko kwa wananchi juu ya hali ya kukatika katika kwa umeme.
Ameyasema hayo wakati alipofanya ziara katika vituo vya uzalishaji umeme kwa njia ya gesi vya Kinyerezi I na II vilivyopo Kinyerezi jijini Dar Es Salaam kujionea hali ya uzalishaji umeme katika vituo hivyo.
Amebainisha lengo la ziara hiyo ni kujionea jitihada zinazifanyika katika kuongeza uzalishaji wa umeme kwa njia ya gesi kama chanzo mseto baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wawekezaji wa viwanda kudai kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa kutokana na upungufu wa umeme.
Sambamba na hilo pia ametoa rai kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira ambao unaweza kuchangia katika uzalishaji wa gesi asilia ambayo itasaidia uzalishaji umeme kuwa mwingi na kutatua changamoto ya upungufu wa umeme ambao unasababishwa mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba dunia na kusababisha vyanzo vya umeme ikiwepo maji kuwa changamoto kupatikana;
“msichoke kutoa elimu kwa watanzania,leo kinachoendelea kwenye maswala ya ukame ni mabadiliko ya tabia nchi na matokeo yake na hii ni kuwaambia tu watanzania kumbe tukitunza vizuri mazingira yetu ndio jambo muhimu ili yaweze kututunza” alisema Mhe.Chalamila.
Pia amewataka wataalam wa TANESCO kuongeza juhudi na ueledi katika kuboresha miundombinu ili kusaidia kupatikana umeme wa uhakika na kuepusha malalamiko toka kwa wananchi.
Kwa upande wake Didas Lyamuya Mkurugenzi wa miradi TANESCO amesema wataendelea kusimamia uboreshaji wa miundombinu ili kuhakikisha umeme unakuwa toshelezi husasani ufungaji wa mitambo ambayo itasaidia kuzalisha umeme zaidi ya megawati 150 katika maeneo hitajika.