Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof.Paschal Ruggajo akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge tuzo ya umahiri kutokana na jitihada za Taasisi hiyo za kuelimisha jamii jinsi ya kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kutoa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo. Kushoto ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Genofeva Matemu akimweleza Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof.Paschal Ruggajo huduma zinazotolewa kwenye banda la Taasisi hiyo wakati wa mkutano wa kimataifa wa kisayansi wa magonjwa yasiyoambukiza unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere.
…………………………..
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
01/11/2023 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea tuzo ya umahiri kutokana na jitihada zake na kuelimisha jamii jinsi ya kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kutoa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo.
Tuzo hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo wakati wa mkutano wa kimataifa wa kisayansi wa magonjwa yasiyoambukiza unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere.
Akizungumza wakati alipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Ruggajo aliipongeza JKCI kwa kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo na hivyo kupunguza asilimia 80 ya wagonjwa wa moyo waliokuwa wakipelekwa na Serikali nje ya nchi kwaajili ya matibabu.
“Ninawapongeza sana kwa kuratibu zoezi la utalii tiba nchini kwani mmekuwa mkipokea wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi ambao wanafika katika Taasisi yenu kwaajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo”, alisema Prof. Ruggajo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt.Peter Kisenge alisema moja ya kipaumbele ambacho Taasisi hiyo imejiwekea ni kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa elimu ya magonjwa ya moyo pamoja na lishe bora kwa wananchi na kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo.
Dkt. Kisenge alisema hadi sasa wameshatoa huduma hiyo ya tiba mkoba katika mikoa zaidi ya 10 na kuwafikia wananchi zaidi ya 7000 na hivi karibuni watakwenda kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika mikoa ya Arusha, Tabora, Kigoma na wilaya za Siha na Kigamboni.
“Huduma hii inajulikana kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ambapo hadi sasa tumeshatoa huduma hii katika mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani na huduma tunazozitoa ni pamoja na elimu ya lishe na matumizi sahihi ya dawa za moyo, uchunguzi na upimaji wa magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kisukari”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema magonjwa yasiyoambukiza yanachangia vifo vingi duniani kote karibu watu milioni 17 wanapoteza maisha yao kutokana na magonjwa hayo.
Katika mkutano huo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatoa elimu ya jinsi ya kuyatambua magonjwa ya moyo pamoja na kueleza huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa.